Hadaa na unyonyaji
Wanawake wengi
Mwanamke anapenda ahisi kuwa yeye ndiye mtu pekee katika maisha ya mwanaume. Kuwa na uhusiano na wanawake wengi wasiokuwa na ukomo, husababisha katika kushusha heshima yake mbele ya mkewe. Tambua kuwa hiyo sio sifa nzuri ya kujivunia.
Uongo
Uongo ni miongoni mwa mambo ambayo mwanamke huchukia sana kuyaona kwa mwanaume. Kuna wanaume hodari katika kutunga na kusema uongo. Lakini mwanamke akigundua kuwa unamuongopea, basi heshima na thamani yako itakuwa imeshuka kabisa machoni mwake hata kama ataamua kuendelea kuishi nawe.
Ukosefu wa heshima
Utovu wa heshima ni miongoni mwa mambo yanayoharibu uhusiano maridhawa baina ya wanandoa hata kama kutakuwa na mambo yanayowaunganisha. Hivyo, ewe mwanaume mwenzangu, usiishushe haiba ya mkeo kwa lugha chafu au kumdhalilisha. Usishushe thamani ya vitu anavyovifanya kwa ajili yake hata kama vitakuwa vidogo. Daima jitahidi kuwaheshimu ndugu zake kwa sababu ukifanya kinyume na hivyo, thamani yako mbele yake itashuka, hata kama hatakwambia.
Kutomuamini
Kuaminiana ni miongoni mwa mambo mazuri ambayo yakipatikana katika mapenzi ya wawili, huwasaidia kukabiliana na vikwazo na changamoto mbalimbali. Ikiwa mume ni mtu anayetilia shaka maneno na matendo ya mke kila siku, thamani yake machoni mwa mkewe itashuka. Kuaminiana kuna mafungamano makubwa sana na upendo na kujiamini. Iwapo kutakuwa na ulegevu katika jambo hilo, mahabba yao hayatakuwa maridhawa.