Asilimia 90 ya barabara zinazosimamiwa na TARURA ni mbaya

Na Hamisi  Abdulrahmani, Masasi

  IMEELEZWA kuwa asilimia 90 ya miundombinu ya mtandao wa barabara zinazosimamiwa na wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) katika Halmashauri ya wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara zipo katika hali ya mbaya ya kutopitika.


  Hayo yalisemwa jana wilayani Masasi na kaimu meneja wa TARURA Halmashauri ya wilaya ya Masasi,John Kimario alipokuwa akijibu hoja za madiwani wa Halmashauri hiyo katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.

  Alisema anakiri kuwa barabara nyingi za Halmashauri hiyo hasa zile zilizopo vijijini kwa sasa zipo katika hali mbaya ya kutoweza kupitika kutokana na kuharibika.

  Kimario alisema changamoto kubwa ambayo inaikabili TARURA kwa sasa ni bajeti inayopewa na serikali kwa ajili ya matengenezo ya barabara kuwa ni ndogo.

   Alisema Halmashauri ya wilaya ya Masasi ina mtandao wa barabara wenye urefu zaidi ya kilometa 1079 lakini bajeti ya TARURA kuufikia mtandao huo ni ndogo hivyo changamoto ya ubovu wa barabara utajitokeza.

   Alisema katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 TARURA ilitengewa bajeti ya matengenezo ya barabara sh.bilioni 1 lakini hadi sasa katika utekelezaji fedha zilizopatikana haziendani na uhalisia wa mtandao wa barabara.

  Alisema  jambo hilo la upatikanaji wa fedha za kutosha linasababisha kuwepo kwa changamoto hiyo ya baadhi ya barabara kushindwa kufikiwa na kufanyiwa matengenezo.

  "Ni kweli asilimia 90 ya mtandao wa barabara katika Halmashauri ya wilaya ya Masasi zipo katika hali mbaya lakini changamoto kubwa ya hili ni ufinyu wa bajeti ...tayari tushapeleka maombi maalumu ya kuomba fedha," alisema Kimario

   Kwa upande wake diwani kata ya Nnavila,Ramadhani Chilumba alisema hali ya barabara za kata hiyo zimeharibika kwa kukatikakatika.

   Naye diwani kata ya Chikolopora, Edward Mahelela alisema ubovu wa barabara kwenye kata zao ni wazi kuwa unakwamisha upatikanaji wa maendeleo ya wananchi.

   Alisema wanaiomba serikali ione uwezo wa kuiongezea bajeti TARURA ili iweze kufanya matengenezo ya barabara kwa ufanisi zaidi.

"Hali ya barabara Halmashauri ya wilaya ya Masasi zipo vibaya baadhi zimekatika madaraja, makaravati na pia zingine hazina mifereji kabisa hivyo mvua zinaendelea kuharibu barabara," alisema Mahelela

  Edger Chilala diwani kata ya Mpanyani, alisema hali ya miundombinu ya barabara za vijijini haihelezeki na pasipo kuchukuliwa hatua ya kuzitengeneza itaendelea kuwakwamisha wananchi.

  Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, ambaye pia ni diwani kata ya Chiungutwa,Juma Satma wao kama madiwani wanaishauri serikali kuiongezea bajeti TARURA kwa vile kata nyingi Masasi barabara zake ni mbovu.