Baba wa Samatta naye awaangukia Watanzania "Tuwe na subira kocha ameliona hilo nafikiri ataliweka sawa"


Baada ya juzi nahodha wa Taifa Stars na mchezaji wa Aston Villa, Mbwana Samatta kuwaangukia mashabiki wake na Watanzania kwa ujumla akiwataka kuacha tabia ya kuandika maneno makali au lugha isiyofaa katika akaunti za wachezaji au klabu hiyo kwa sababu hali hiyo inamkera, hatimaye baba yake mzazi naye ametoa raia hiyo.

Mzee Samatta alisema, ni kweli wachezaji wa Aston Villa michezo yote miwili waliyoicheza walionekana kutotoa pasi kwa Samatta, lakini aliwataka Watanzania wavute subira pamoja na kuacha kuandika maneno ya ubaguzi, ambayo yanaweza kumpa wakati Samatta Jr wakati mgumu.

Alisema Samatta Jr ni mpambanaji, hivyo atakuwa kinara tu wa kufunga mabao, jambo ambalo aliwataka Watanzania wenzake kuwa na subira.

"Nimekasirishwa sana kuona maneno yaliyoandikwa kwenye ukurasa wa Aston Villa ambayo yamekandia wachezaji wenzake, si kitu kizuri, tusubiri tuone kwa sababu kocha wake ameliona hilo nafikiri ataliweka sawa, alisema Mzee Samatta.

Alifafanua kuwa hali hiyo pia aliwahi kumkumba Samatta Jr wakati alipojiunga na TP Mazembe na kisha KRC Genk ya Ubelgiji, lakini baadaye alikuwa mchezaji mzuri, hivyo jambo linalohitaji subra tu.

"Hiyo ni moja ya changamoto kwa Samatta anatakiwa akumbuke amevuka vitu vingapi mpaka kufika alipo sasa, naamini yatapita atakaa sawa kwa sababu kipaji anacho," alisema.

Alisema tangu mwanawe aandike ujumbe huo kwenye ukurasa wake, hajazungumza naye kitu chochote zaidi ya kumpongeza jinsi alivyocheza.

"Mimi nilimpongeza tu jinsi alivyocheza, lakini sijazungumza naye chochote juu ya hilo lililojitokeza," alisema huku akimtakia kila la heri katika maisha mapya ya soka, na kumtaka aongeze bidii asikatishwe tamaa na changamoto hizo.