Balozi Kanali Ibuge akutana, kufanya mazungumzo na Sekretarieti ya SADC


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Pamoja na mambo mengine, Katibu Mkuu alipokea taarifa ya ziara ya Sekretarieti ya SADC na kuwahakikishia ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kufanikisha mikutano yote ya SADC kipindi cha Uenyekiti wa Tanzania.


Ujumbe wa Sekretarieti ya SADC unaongozwa na Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa SADC, Bibi. Bodo Tanrely Radaody Ravarosy ambao wapo nchini kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa SADC unaotarajiwa kufanyika tarehe 10 – 11 Machi, 2020, Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, ujumbe huo ulipata fursa ya kukutana na Katibu Mkuu Balozi Ibuge na kumpa taarifa ya maandalizi ya mkutano huo.

Mwezi Augosti, 2019 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alipokea rasmi Uenyekiti wa SADC katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wanachama.

Aidha, hatua hiyo ilifuatiwa na mikutano mbalimbali ya kisekta iliyofanyika na inayoendelea kufanyika hapa nchini kwa kipindi cha kuanzia mwezi Septemba 2019 hadi Agosti, 2020 ambapo hadi sasa imeshafanyika mikutano mitatu ya kisekta.


Mikutano hiyo ni pamoja na Mkutano wa Mawaziri wa SADC wenye dhamana ya masuala ya Tehama, Habari, Uchukuzi na hali ya Hewa, Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa Sekta ya Afya na VVU na UKIMWI pamoja na mkutano wa pamoja wa Mawaziri wa Mazingira, Maliasili na Utalii.