Chato: Baba Kizimbani kwa Kumlawiti Mtoto Wake

Jeshi la Polisi wilayani Chato mkoani Geita, limemfikisha Mahakamani, Kazimili Dotto akituhumiwa kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa kambo, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili.

Mwendesha Mashtaka Mauzi Lyawatwa, amesema kosa la ubakaji ni kinyume na Vifungu vya 130(1)(2)(e) na 131(1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai.

Februari 17, 2020 Mshtakiwa akiwa nyumbani kwake, alimwita mtoto huyo na kumwomba amletee maji ya kunywa ndani ya chumba anacholala na mkewe kabla ya kumbaka na kumlawiti.

Inadaiwa baada ya mtoto huyo kufikisha maji, alikamatwa kwa nguvu na kutupiwa kitandani na baba yake ambaye alimvua nguo za ndani na kuanza kumbaka na kumlawiti.

Inaelezwa kuwa Mama wa mtoto alikuwa shambani na aliporejea, alisukuma mlango wa chumba chake uliokuwa umeegeshwa, kisha kumkuta mumewe akitenda unyama huo.

Baada ya kutolewa maelezo hayo na Upande wa Jamhuri, Mshitakiwa alikana kuhusika na mashtaka yanayomkabili. Hakimu Mkazi Mfawidhi Odira Amworo, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 24 mwaka huu.