https://monetag.com/?ref_id=TTIb Jafo ampongeza Mavunde kwa kujenga shule itakayomaliza changamoto ya umbali mrefu kwa wanafunzi | Muungwana BLOG

Jafo ampongeza Mavunde kwa kujenga shule itakayomaliza changamoto ya umbali mrefu kwa wanafunzi

Serikali imesema mwisho wa wanafunzi wanaotembea umbali mrefu kwenda shule katika kata ya Nala jijini Dodoma ni mwaka huu kwani kuanzia mwakani hakutakua na changamoto ya madarasa katika shule ya msingi kwenye kata hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mhe Selemani Jafo wakati akizindua shule shikizi ya msingi ya Chiwondo iliyopo katika Jiji la Dodoma.


Shule hiyo imejengwa kwa msaada wa Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mhe Anthony Mavunde kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji hilo ambapo tayari vyumba vinne vya madarasa vimeshakamilika huku vingine vitatu vikiwa kwenye ujenzi.

Akizungumza na viongozi, wananchi na wanafunzi waliojitokeza kwenye uzinduzi huo, Mhe Jafo amemuagiza Mkurugenzi wa Elimu-Tamisemi, Bw Julius Nestory kuhakikisha Shule hiyo inaongezewa madarasa mawili kabla ya kuanza kwa Bunge lijalo la bajeti.

" Kazi kubwa ambayo imeoneshwa na Mbunge wenu inapaswa kuungwa mkono na kila mmoja wetu, hivyo nakuagiza Mkurugenzi wa Elimu uhakikishe ujenzi wa madarasa mawili unaanza mara moja kabla ya bunge la bajeti kuanza.

Hatuwezi kumuachia  Mbunge peke yake kazi ya kuleta maendeleo, lakini pia nakuagiza Mkurugenzi uhakikishe katika ajira zijazo za serikali Shule hii inapata walimu na kuondoka na na changamoto ya walimu iliyopo," Amesema Mhe Jafo.

Amesifu jitihada kubwa zilizooneshwa na Mbunge Mavunde za kuinua elimu kwenye jimbo lake na kuwataka wananchi, wazazi kukubaliana nae kuiita shule hiyo jina la Mavunde.

" Mimi hizi shule zipo kwenye mamlaka yangu nimesikia mnasema inaitwa Chiwondo mimi naagiza isajiliwe kwa jina la Mavunde, hii ndiyo heshima pekee ambayo tunaweza kumpa Mbunge wetu," Amesema Jafo.

Kwa upande wake Mhe Mavunde amemshukuru Waziri Jafo na viongozi wengine waliofika kwenye uzinduzi huo kwani kukamilika kwa shule hiyo kumepunguza changamoto ya umbali mrefu iliyokua ikiwakabili wanafunzi hao.

" Mhe Waziri kabla ya shule hii iliwalazimu wanafunzi hawa watoto kutembea Km 20 kila siku kwenda na kurudi shuleni, jambo ambalo kwa hakika lilisababisha wengi wao kuacha shule na wengine kufanya vibaya kutokana na uchovu wanaoupata," Amesema Mavunde.


Akizungumza mara baada ya kuzinduliwa kwa shule hiyo mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Anneth Jacob amemshukuru Mhe Mavunde kwa kuwaletea shule hiyo kwani anaamini itakua safari ya wengi kutimiza ndoto zao za kimasomo na kimaisha.

Kufunguliwa kwa shule hiyo shikizi kumeongeza idadi ya wanafunzi waliojiunga na elimu ya awali kutoka 15 waliokua wakisoma Chihoni hadi 63 sasa wanaosoma Chiwondo.