Waziri Simbachawene awataka watendaji wakuu Polisi kuwahoji watuhumiwa waliopo mahabusu za Polisi nchini

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewataka Watendaji Wakuu wa Jeshi la Polisi wawahoji watuhumiwa waliopo katika mahabusu ya vituo vya polisi nchini ili kujua makosa waliyoyafanya kama wanastahili kuwepo katika mahabusu hizo.

Waziri Simbachawene amesema lengo lake kuu la agizo hilo ni kudhibiti ubambikizwaji kesi ambao upo katika vituo mbalimbali nchini ambapo baadhi ya watuhumiwa wanapelekwa magerezani kwa makosa ambayo hawakuyafanya.


Akizungumza katika kikao chake na Watendaji hao kilichofanyika ukumbi wa ofisi ndogo ya Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dar es Salaam, leo, Waziri Simbachawene alisema maelekezo yake pamoja na ya Rais John Magufuli yanahusu masuala ya kesi na ubambikizaji wa kesi ambayo yapo katika baadhi ya vituo vya Polisi nchini.

“Nawataka mfanye mchujo katika kesi za watuhumiwa mbalimbali waliopo mahabusu  ambazo zinapelekwa mahakamani watuhumiwa hao wanafanyiwa ‘screening’ hata mara mbili au tatu kwa kuwahoji makosa yao uso kwa uso ili kuhakikisha mtuhumiwa huyo ndiye mwenye kesi ya mauaji, au anakesi ya kubaka, au anakesi ya wizi, na hata akipelekwa mahakamani awe ndiye anayestahili,” alisema Simbachawene.

Simbachawene ameongeza kuwa, kunaweza kutokea wakati mwingine mtuhumiwa anakuwa na kesi nyingine lakini anapewa kesi ambayo hastahili na m tuhumiwa huyo anashangaa kwa kuwa sio kosa alilolitenda ambalo kakamatwa nalo.

Pia Waziri Simbachawene, aliwataka Viongozi hao wa Polisi kusimamia kwa hekima na busara suala la vijana wengi wanaoendesha bodaboda, kwa kuwa ni kundi kubwa na vijana ambao wamejiajiri kwa lengo la kupambana na ukosefu wa ajira nchini na duniani kwa ujumla.

“Isitafsiriwe kwamba ukiwaona vijana waenda bodaboda ni watu wa hovyo hovyo, waendesha bodaboda wapo wenye digrii, diploma, kidato cha sita, wenye vyeti, wapo kidato cha nne, sio kundi la hovyo kama wanavyofikiri baadhi ya watu, hawa ni watu waliojiajiri na wanafanya shughuli zao kihalalikwa mujibu wa sera za nchi, kwa hivyo ni lazima tutambue mchango wao na pia tutambue changamoto zao,” alisema Simbachawene.

Alisema Jeshi la Polisi linapaswa kuwa makini, na litumie busara na uadilifu na pia liwe na huruma katika kuwaangalia vijana hao waendesha bodaboda ambao wanahangaika kutafuta riziki na kuendesha maisha yao.

Aliongeza kuwa, Taifa na dunia kwa ujumla kuna ukosefu mkubwa wa ajira hivyo kunapotokea vijana wanajiari lazima eneo hilo litunzwe na lipendwe na sio kupachukulia eneo la kukomeshana kwa kuwanyanyasa na kuwafanya kama hawatakiwi katika jamii.

Aidha, Waziri Simbachawene aliwataka watendaji hao waendeleze ushirikiano walionao ili kuweza kupata njia ya mafanikio zaidi katika utendaji wa Jeshi hilo.

“Hii nyimbo yenu ya maadili kwa kweli nimeependa, na ninatamani kila mwananchi ajifunze, ni mzuri na unalengo jema, hivyo wimbo huu nawataka muuishi kutokana na wimbo unavyotaka, lazima tuwe na maadili mema na tuliendeleze Jeshi letu la Polisi,” alisema Simbachawene.

Kwa upande wake, Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro, alimshukuru Waziri huyo kwa kufanya kikao na viongozi wa Jeshi lake, na alimuahidi kwa kushirikiana na viongozi wenzake, watayafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa.

“Tumefurahi kumpokea Mheshimiwa Waziri hapa Makao Makuu Madogo ya Polisi, ni mara ya kwanza kufika hapa, na pia amezungumzia mambo mengi, yakiwemo maadili ya kazi, na pia amezungumza masuala ya uhalifu, amesema tupambane na uhalifu mapema kwa kuzuia kabla ya kutokea, na pia amezungumza masuala ya kushirikiana ndani ya Jeshi, na pia amezungumzia masuala ya bodaboda, na tunaahidi maagizo yote aliyoagiza tutayafanyia kazi,” alisema Sirro. 

Waziri Simbachawene tangu ateuliwa na Rais Magufuli kuiongoza Wizara hiyo, baada ya aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, kangi Lugola, kuondolewa katika nafasi hiyo, ameanza ziara ya kutembelea taasisi za wizara yake ambazo ni Jeshi la Polisi, tayari amezungumza nao, na anatarajia kufanya kikao na Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.