Maambukizi ya Corona yaongezeka Korea Kusini, Italia na Iran zachukua hatua zaidi

Korea Kusini imeripoti ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya Corona 123 na kufanya walioambukizwa kufikia 556, wakati Italia na Iran zikichukua hatua zaidi za kukabiliana na mripuko huo. Idadi ya vifo nchini Korea Kusini nayo imeongezeka hadi kufikia watu wanne.

Siku ya Ijumaa Italia ilikuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kuripoti kuwa raia wake mmoja amefariki kutokana na Corona na kufuatiwa na kifo kingine jana Jumamosi. Zaidi ya raia 50,000 katika miji kadhaa ya Kaskazini mwa Italia wameamuriwa kusalia nyumbani wakati maduka na shule vikifungwa.

Iran nayo imezifunga shule, vyuo na vituo vya utamaduni katika majimbo 14 hii leo kufuatia vifo vya watu watano.

Ingawa Misri ndio taifa pekee afrika ambalo limethibitisha kisa cha COVID-19, lakini shirika la afya ulimwenguni WHO limeonya kuwa mifumo ya afya Afrika sio imara kuweza kukabiliana na miripuko mikubwa na kuomba ushirikiano zaidi ndani ya Umoja wa Afrika.