Walimu Mbwara wachangishana milioni 3 kuweka umeme



Na Omary Mngindo, Mbwara

Walimu wa shule ya Sekondari ya Kata ya Mbwara jimbo la Rufiji Mkoa wa Pwani, wamejichangisha shilingi milioni tatu kwa ajili ya kuweka umeme kwenye nyumba wanazoishi sanjali na vyumba vya madarasa.

Hayo yamo katika taarifa iliyosomwa na Mwalimu Mkuu shuleni hapo Millo Msovela, mbele ya Mbunge wa jimbo la Rufiji Mohamed Mchengerwa, akiwa na wa Viti Maalumu Zaynab Vulu, iliyoelezea kuwa sasa changamoto ya kukosekana kwa huduma hiyo imebaki katika mabweni ya wasichana.

Taarifa imefafanua kuwa hatua hiyo imetokana na mafundi wa Tanesco kufika kijijini hapo na kuweka miundombinu hiyo, wakati shule ambapo shule ikiwa haina pesa, hali iliyowalazimu kujichangisha kiasi hicho cha fedha kilichowezesha kuwekwa katika nyumba zao na madarasani.


"Pamoja na juhudi hizo za walimu za kiweka umeme katika nyumba zetu na kwenye madarasa, bado kuna changamoto ya kukosekana kwa nishati hiyo kwenye mabweni ya wasichana, kutokana na kukosa shilingi laki nne za kuumganishia huduma hiyo," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Imeongeza kwamba pia shule inadaiwa shilingi milioni kumi na Mzabuni aliyetengeneza vitanda 40 vitavyoliwa na wanafunzi 80 wa kike, kati ya 188 waliopo shuleni hapo ukiachilia wavulana 162 wanaosoma kwenye shule hiyo ambapo wanatokea majumbani mwao.


Akizungumza na walimu, wanafunzi, wazazi na viongozi waliofika shuleni hapo, Mchengerwa alipongeza hatua ya walimu kujichangisha fedha na kuvuta umeme, huku akiahidi kushirikiana na.viongozi wemzake ili kurejesha fedha hizo.

"Katika taarifa ya mwalimu imegusia changamoto kadhaa ikiwemo deni la vitanda, nitawasiliana na Taasisi ya TEA iliyoratibu mradi husika, kuhusu umeme katika mabweni nimewasiliana na Meneja wa Tanesco ameniahidi ndani ya simu 14 utawaka," alisema Mchemgerwa.

Nae Zaynab Vulu kabla ya kwenda kukabidhi vifaa tiba kwenye zahanari ya Kijiji cha Mbwara, akiwa shuleni hapo alikabidhi magodoro kumi, huku akiahidi mifuko mitano ya saruji akiunga mkono mofuko 15 iliyoaihidiwa na Mchengerwa kwa lengo la kukarabati sakafu kwenye majengo shuleni hapo.

Vulu aliwataka wanafunzi shuleni hapo kuzingatia masomo, huku akiwanyooshea kidole wasichana, kuwa makini na kutokubalu kirubuniwa na vishawishi kutoka kwa wavulana kwani vitawakatishia masomo, hivyo kupoteza malengo yao.

Akikabidhi vifaa tiba kikiwemo kipimo cha presha, kisukari, shuka pamoja na kikinga sare ya kazi (Apron), Vulu alisema kwamba ameungana na juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya afya, ambapo kwa uchache wake nae ameunga mkono kwa vifaa hivyo.