Marekani yatafuta washirika wa kushindana na Huawei

Mwakilishi maalumu wa ikulu ya White House kuhusiana na masuala ya sera za mawasiliano ya kimataifa ya simu Robert Blair, amesema Marekani inataka kuunda ushirikiano na kampuni za mawasiliano ya simu kutoa mbadala kwa teknolojia za Huawei kutoka China.

Akizungumza katika Kongamano la Usalama la Munich nchini Ujerumani, Blair alisema ushirikiano ni tofauti na kununua hisa kwa kutumia pesa za umma.

Awali, Mwanasheria Mkuu wa Marekani William Barr alikuwa amependekeza kwamba Marekani ilikuwa inakadiria kuchukuwa udhibiti wa washindani wawili wakuu wa kimataifa wa Huawei ijapokuwa baadaye ikulu ya White House ilifutilia mbali mapendekezo hayo.

Blair pia alisema Uingereza ilihitajika kuangazia kuhusu uamuzi wake wa kutumia kifaa kilichotengenezwa na Huawei ambacho maafisa wakuu nchini Marekani wanasema ni tishio la usalama, madai yaliokanushwa na kampuni hiyo.