Mkurugenzi wa Zahanati ya Margakan atolea ufafunuzi tuhuma za kuwatoza fedha Wajawazito



Na John Walter-Babati

Kufuatia baadhi ya wajawazito mjini Babati wanaofika kupata huduma ya Kliniki katika Zahanati ya Margakan, kulalamika kutozwa fedha,Mkurugenzi wa Zahanati hiyo Nikodemus Kaje amedai kuwa madai hayo sio ya kweli.

Ikumbukwe kwamba Serikali hutoa bure huduma ya Kliniki.

Dk. Nicodemus Kaje alisema wajawazito hawalipii huduma hiyo bali kuna kipimo cha kusikiliza mapigo ya mtoto tumboni ndicho wanalipia sh. 2,000 ambacho ni mbadala wa mashine ya utra sound ambayo ni gharama kubwa ila hicho kipimo ni kwa hiari siyo lazima na siyo kila siku.

Kuhusu watoto kupima uzito Dk. Kaje alikiri kuwatoza sh. 500 ili huduma hiyo ijiendeshe kutokana na wao kupewa jokofu la kuhifadhia dawa ambapo linatumia umeme mwingi na wao hawana chanzo kingine cha kulipia umeme huo hivyo waliona sh. 500 ndio isaidie.

Aidha alisema huduma za watoto na wajawazito zinaenda vizuri ambapo kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita watoto 381 walipata chanjo, watoto 1601 walipimwa uzito na wajawazito 483 walipatiwa huduma katika zahanati hiyo na kusaidia kupunguza msongamano Hospitali ya Mrara.

Aidha alisema siyo kwamba wajawazito ndio wanatozwa fedha tu hata watoto wadogo kupimwa uzito nao wanalipia sh. 500.

Aliwataka kuacha kulalamika kwa kua utoaji wa huduma hiyo unawaondolea usumbufu wa kutumia gharama za usafiri na kukaa kwenye foleni muda mrefu.

Aliongeza kuwa serikali itakapowasainisha mkataba wa utoaji huduma ndio utasaidia kuondoa baadhi ya changamoto.

Mmoja wa wajawazito aliyezungumza  kwa sharti la kutokuandikwa jina alisema Margakan wanawatoza sh. 2000 kila mjamzito anapohudhuria kliniki kila mwezi.

"Kiukweli tumechoka kulipa fedha hii mbona zahanati zingine za binafsi hawawatozi fedha iweje hapa wanatutoza fedha,"Alihoji mjamzito huyo

Mjamzito mwingine ambaye naye alitoa sharti la kutokufahamika jina lake alisema anashangazwa na zahanati hiyo ya binafsi kuwatoza fedha tofauti na maeneo mengine.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items