Mwakalinga aiagiza TANROADS kukarabati barabara ndani ya siku mbili

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo, Elius Mwakalinga, amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS),Mkoa wa Mbeya, kuhakikisha ndani ya siku mbili anakarabati maeneo yote korofi yaliothiriwa na mvua katika barabara ya Isyonje- Makete (Km 96.4) ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.

Mwakalinga, ametoa agizo hilo mkoani Mbeya wakati alipokuwa akikagua athari za mvua katika miundombinu ya barabara hiyo inayounganisha mkoa wa Mbeya na Njombe akiwa katika kijiji cha Igoma, ambapo amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu kwani ni kiungo cha mawasiliano
kati ya mikoa hiyo miwili.

“Hakikisha Meneja, barabara hii inapitika ifikapo kesho, kusanya wataalamu wako wote waliopo katika mkoa wako, mje hapa kufanya kazi ili kuhakikisha barabara hii inarudi katika hali yake ya awali” amesema Mwakalinga.

Amesisitiza kuwa licha ya mvua kuendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo lakini bado wananchi wanahitaji hali nzuri ya barabara ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria na mazao kutoka sehemu mbalimbali.

Mwakalinga, amefafanua kuwa ameamua kufanya ziara hiyo ili kubaini athari za mvua katika miundombinu ya barabara na kutatua changamoto zake pamoja na kuangalia maendeleo ya miundombinu hiyo katika
maeneo mbalimbali nchini ili kuzipa kipaumbele katika kuzitengea fedha barabara zote zenye changamoto kwenye bajeti ijayo.

“Kama mnavyojua kipindi cha bajeti kimekaribia, sasa ni muhimu kuzikagua barabara hizi ili nione namna ya kuzipa kipaumbele kwa kuziwekea fedha katika bajeti ijayo kwa barabara zote ambazo zina changamoto”, amefafanua Mwakalinga.



Kwa upande wake, Meneja Wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Eliazary Rweikiza, amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa atakarabati kwa wakati barabara hiyo na kuhakikisha inapitika majira yote ambapo ameongeza kuwa tayari mkandarasi ameshaaanza kurekebisha sehemu zilizoharibika na kwamba ndani ya siku mbili kazi zote zitakuwa zimekamilika na barabara kupitika.



Katika hatua nyingine, Mwakalinga, amekagua barabara ya Njombe- Ndulamo – Makete sehemu ya Moronga – Makete (Km 53.5) ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi M/s China Railway Seventh Group.



Mwakalinga, amemtaka Mkandarasi huyo kuendelea na ujenzi kwa kazi ambazo zinaweza kufanyika katika kipindi hiki cha mvua ili mradi ukamilike kwa muda uliopangwa kulingana na mkataba.



Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe, Mhandisi Yusufu Mazana, amemhakikisha Mwakalinga kuwa atamsimamia mkandarasi huyo ili aweze kukamilisha kwa wakati kwani mradi huo ni muhimu katika usafirshaji wa mazao ya misitu, chakula pamoja na utalii.