Njombe: Wazidi kulia na ugumu wa biashara


Na Amiri kilagalila,Njombe

Hali ya biashara kwa wakazi wa mji wa Njombe imetajwa kuwa kwenye mkwamo kutokana na Ongezeko la kodi hasa katika ukadiriaji wa kodi hatua inayowalazimu baadhi ya wafanyabiashara kufunga milango yao.

Katika mkutano wa kwanza mwaka 2020 wa jumuiya ya wafanyabiashara mjini Njombe,baadhi ya wafanyabiashara akiwemo Agnetha Sanga na Nathaniel mgani wanakiri kuwa hali ya biashara kwa sasa imekuwa ngumu na mauzo kupungua kwa kiasi kikubwa.

Kutokana na hali hiyo serikali inaombwa kuangalia namna ya kuwapunguzia mlundikano wa kodi kwani hakuwezi kuwa na makusanyo makubwa ya mapato ilihali biashara hakuna.

"Kwanza tozo kwa kweli imekuwa ni kubwa kuliko vipato,kwa hiyo utakuta ni wafanyabiashara wachache sana leo watakwambia nimeuza na wengine wameamua kufunga milango kwasababu biashara hamna,leo sio sawa na miaka iliyopita angalau tulikuwa tunasema tunafanya kazi"aliseama mmoja wa wafanyabiashara

Eliud Mgeni[Pangamawe] ni mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoa wa Njombe anasema bado wafanyabaishara wanayo nafasi ya kujitoa walipo kwa kuongeza usimamiaji wa biashara zao badala ya kukata tamaa.

"Kwa mwaka huu tunaomba TRA kuwa na sababu ya kuhakikisha wafanyabiashara wote wanalipa kodi kwa hiali zinazolipika bila ya kuwa na maumivu,mapato ya kodi ya serikali tunalipa faida inayotokana na biashara kwa hiyo kama hujapata faida unaenda kulipa nini"alisema Pangamawe

Kwa upande wake meneja wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Njombe Musibu Shaaban anasema makadirio ya kodi yanafanyika kulingana na mauzo na hivyo ili kuondoa malalamiko hayo ndiyo maana wanaendelea kusisitiza kutumia mashine za EFD.

"sisi kama TRA huwa tunakadiria kulingana na mauzo ya mtu,kwa hiyo swala lakusema biashara imekuwa ngumu hilo siwezi kuzungumzia lakini cha msingi kama mtu biashara yake imeshuka kidogo lazima mauzo yaonekana na ndio maana tunasisitiza sana watu watumie mashine za EFD kwasababu zinaonyesha kila kitu"alisema Musib Shaaban.


Jumuiya ya wafanyabiashara mji wa Njombe imetoka na maadhimio mbalimbali ikiwemo kwenda kujiweka sawa kiuongozi na kusajili wanachama wote ambao watakuwa na nguvu ya pamoja katika kusogeza mbele uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja.