Rais wa Togo ashinda tena uchaguzi


Rais Faure Gnassingbe wa Togo amechaguliwa tena kwa asilimia 72 ya kura, kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi wa nchi hiyo hivi leo.

 Matokeo hayo yanampa nafasi ya kuongoza tena kwa muhula mwengine, baada ya kutawala kwa miaka 15 kutokea mwaka 2005.

Pia yanaendeleza utawala wa familia ya Gnassingbe kwenye taifa hilo la magharibi mwa Afrika.

 Faure alichukuwa madaraka kutoka kwa baba yake, Gnassingbe Eyadema, aliyeingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 1967 na kufariki dunia mwaka 2005.

 Licha ya maandamano makubwa ya kumtaka aondoke madarakani, upinzani uliosambaratika umeshindwa kumzuwia kiongozi huyo mwenye miaka 53 kurejea madarakani kwenye taifa hilo dogo lenye raia milioni nane.