Safari za ndege zafutwa Ujerumani kutokana na kimbunga


Mamia ya safari za ndege zimefutwa nchini Ujerumani kutokana na kimbunga kikali cha msimu wa baridi ambacho kimeleta shida kaskazini mwa Ulaya, huku maelfu ya nyumba zikiachwa bila umeme kutokana na upepo mkali na mvua kubwa.

Uwanja wa ndege wa Munich ndiyo umeathirika zaidi, huku msemaji wake akisema safari 420 za ndege zimefutwa.

Shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa, limeahirisha safari za ndani ya bara la Ulaya hadi saa saba mchana wa leo na ndege zinazoenda nje ya bara la Ulaya hadi saa nane mchana.

Kiasi cha safari 150 za ndege zimefutwa kwenye viwanja vya Duesseldorf na Cologne, huku nyingine kadhaa zikifutwa Stuttgart na Hamburg.

Kimbunga hicho kinachojulikana kama Sabine nchini Ujerumani na Ciara kwenye nchi nyingine, pia kimeleta madhara nchini Uingereza, Ireland na Ufaransa.