Hofu imeongezeka leo kuhusu janga la ugonjwa wa virusi vya Corona baada ya kuongezeka kwa visa vipya vilivyoripotiwa nchini Iran, Italia na Korea Kusini lakini China imelegeza vikwazo vya kutembea katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na Beijing huku viwango vyake vya maambukizi mapya vikipungua
.Kuongezeka kwa visa vya maambukizi nje ya China bara kumechochea kuporomoka kwa hisa za Asia katika masoko yake na katika soko la hisa la Wall street huku wawekezaji wakikimbilia kuwekeza katika vitu salama kama dhahabu.
Mji wa Daegu nchini Korea Kusini umeendelea kutengwa huku idadi ya maambukizi ikiongezeka katika eneo hilo na mashirika ya ndege ya Asiana na Korea yakiahirisha safari zake za ndege katika mji huo hadi Machi 9 na 28 mtawalio.
Kwa mujibu wa naibu waziri wa afya wa Korea Kusini, Kim Kang-lip, amewaambia wanahabari kuwa iwapo hawataweza kudhibiti kusambaa kwa kirusi hicho katika eneo la Daegu kwa njia bora, kuna uwezekano kikasambaa kote nchini humo.
