UWT Ilemela wampongeza Dk. Angeline Mabula


Na James Timber, Mwanza

Baraza la Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela wamempongeza Mbunge wa Jimbo hilo Dkt Angeline Mabula kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa kipindi cha 2015-2020.

Pongezi hizo zimetolewa na wajumbe wa kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Ilemela Bi Salome Kipondya kikiwa na lengo la kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 kutoka kwa madiwani wa Viti maalum  wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi ndani ya manispaa ya Ilemela ambapo amesema kuwa Baraza hilo kwa pamoja linaridhishwa na taarifa zilizowasilishwa na madiwani sita wa Viti maalum akiwemo Mhe Rosemary Mwakisalu, Denisa Pagula, Saphia Mkama, Elizabeth Wangaruke, Kuruthumu Abdalla na Rahma Hilal juu ya uwajibikaji wao kwa wananchi sambamba na kumpongeza mbunge wa jimbo hilo kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha anawatumikia wananchi wake na kuwaletea maendeleo kwa kukamilisha kwa zaidi ya asilimia 95 ya Ilani ya uchaguzi huku wakitaja miradi iliyotekelezwa ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya Karume, kituo cha afya Buzuruga, hospitali ya wilaya, ujenzi wa barabara ya Sabasaba-Kiseke-Buswelu, barabara ya Nyakato Steel-Buswelu na zile za kipindi cha mkoloni zilizokuwa hazifunguki kwa fedha za mfuko wa jimbo, ukarabati na ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari ikiwemo Angeline Mabula sekondari,ujenzi wa miradi mikubwa ya maji ikiwemo tanki kubwa na la kisasa la kusambaza maji Nyasaka, tanki la Nyamadoke, chanzo cha maji Igombe, kuendesha zoezi la upimaji na urasimishaji makazi.

"Napenda kutumia fursa hii kumpongeza mbunge wa jimbo letu Dkt Mabula kwa kweli mwanamke mwenzetu huyu anafanya kazi, Sisi kama wanawake wenzie tunajivunia uwepo wake na tutaendelea kumuunga mkono kwa kazi anazofanya," alisema mwenyekiti huyo

Kwa upande wake katibu wa jumuiya hiyo Bi Salama Mhampi amewataka viongozi hao kutimiza wajibu wao ikiwa ni pamoja na kujiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 pamoja na kufanya tathimini za uchaguzi wa Serikali za mitaa uliokwisha ambapo chama hicho kilipata ushindi wa kishindo kwa kushinda mitaa yote 171 iliyopo ndani ya jimbo la Ilemela.

Baraza la Umoja wa Wananwake wilaya ya Ilemela lilihudhuriwa na katibu wa UWT mkoa wa Mwanza Bi Mary Mhoha, Mbunge wa Viti maalum Mhe Koshuma Kiteto, Katibu wa CCM Ilemela Bi Aziza Isimbula, Baadhi ya wajumbe wa kamati ya utekelezaji na baraza kutoka mkoa wa Mwanza.