Virusi vya corona: Mwanafunzi wa Cameroon asimulia alivyopona

Kabla Kem Senoua Pavel Daryl, mwenye umri wa miaka 21-ambaye ni mwanafunzi raia wa Cameroon anayeishi katika mji wa Jingzhou, kuambukizwa virusi vya corona, hakuwa na mpango wa kuondoka China, hata kama hilo lingewezekana.

"Chochote kitakachofanyika sitaki kupeleka ugonjwa Afrika," alisema akiwa katika chumba chake cha malazi katika Chuko Kikuu, ambako ametengwa kwa siku 14.

Alikuwa anaugua homa kali, kukohoa vibaya na kuonyesha dalili za mafua. Alipokuwa mgonjwa alikumbuka jinsi alivyopata malaria akiwa mtoto Cameroon. Alihofia sana maisha yake.

"Nilipokuwa nikienda hosipitali kwa mara ya kwanza nilikuwa nikiwaza kifo na jinsi ambavyo huenda ikanitokea," alisema.

Kwa siku 13 alitengwa katika hospitali moja nchini China.

Alitibiwa kwa antibiotiki na dawa za kutibu wagonjwa walio na virusi vya Ukimwi, HIV. Baada ya wiki mbili ya uangalizi alianza kuonesha dalili ya kupona.

Uchunguzi wa kimatibabu wa CT scan haukuonesha dalili zozote za ugonjwa.

Alikuwa mtu wa kwanza mwenye asili ya kiafrika aliyepona baada ya kuambukizwa na virusi hatari vya corona.China aligharamia matibabu yake.

Misri ni nchi ya kwanza ya Afrika kuthibitisha kisa cha maambukiza ya virusi vya corona.

Wataalamu wa Afya wameonya kuwa nchi zlizo na mifumo hafifu za matibabu huenda zikakabiliwa na changamoto ya kukabiliana na mlipuko wa virusi hivyo, ambavyo vimesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,600 na wengine zaidi ya 68,000 kupata maambukizi wengi wao nchini, China.

"Sitaki kurudi nyumbani kabla nikamilishe masomo yangu. Nadhani hakuna haja ya kurudi nyumbani kwasababu gharama zote za hospitali zimesimamiwa na serikali ya China," alisema Bwana Senoua.