Watakaozembea mradi wa uboreshaji umeme Dodoma waonywa

Serikali kupitia wizara ya Nishati, imewaonya wale wote watakaosababisha mradi wa uboreshaji umeme Dodoma kushindwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, watachukuliwa hatua, kwa sababu hakuna sababu za msingi mradi huo usikamilike.

Akitembelea kituo cha kupoozea umeme cha Zuzu Dodoma, Waziri wa Nishati Dkt. MEDARD KALEMANI, amesisitiza kuwa hakuna muda wa kuongeza kukamilisha mradi huo, ambao unahitajika kwa haraka, baada ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.

Mbali ya kuonya kuchukua hatua, waziri huyo wa Nishati, akachukua wasaa huo kufafanua ni kwa nini wanahimiza mradi huo ukamilike mwishoni mwa mwezi huu.

Mradi huo wa kuboresha kituo cha kupoozea umeme, ulianza mwezi Machi mwaka 2018, na unatekelezwa na Mkandarasi KEC Internatioanl Ltd, chini usimamizi wa Mkandarasi Mshauri Intec na Shirika la Umeme nchini (TANESCO), ambapo serikali imetoa dola milioni 52, kwa ajili ya kutekeleza mradi huu.