Yanga yaonywa, Prisons yapewa ushindi wa mezani


Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake cha Februari 13, 2020 ilipitia taarifa mbalimbali za mechi ya Ligi Kuu Vodacom (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL) zinazoendelea hivi sasa.

LIGI KUU
Mechi namba 197- Singida United FC 2 vs Mwadui FC 2. Mchezaji wa Mwadui Hashim Yahya Mussa amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kwa kosa la kuwaonyeshea kidole cha kati watazamaji kama ishara ya matusi baada ya filimbi ya kumaliza mchezo ilipopigwa.kitendo hicho kilifanyika katika mchezo uliofanyika February 8, 2020 katika uwanja wa Namfua mjini Singida.

Mechi namba 200- Ruvu Shooting 0 FC vs Yanga SC 1-Timu ya Yanga SC imepewa Onyo kali kwa kosa la kuwakilishwa na watu pungufu ya idadi inayotakiwa katika kikao cha maandalizi ya mechi (Pre-match meeting) na kujaza jina la Kocha wa walinda milango Peter Manyika kuwa amehudhuria kikao hicho wakati hajahudhuria .Kitendo hicho kilifanyika katika maandalizi ya mchezo uliofanyika February 08, 2020 katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Onyo kali limetolewa kwa uzingativu wa kanuni ya 34 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Mechi namba 205- Ruvu Shooting vs Tanzania Prisons FC. Tanzania Prisons FC imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kwenye mchezo uliokuwa ufanyike Februari 11, 2020 baada ya timu ya Ruvu Shooting FC ambayo ndiyo timu mwenyeji kushindwa kuleta gari la wagonjwa (Ambulance) uwanjani kama Kanuni ya 14 (2l) inavyosema na kusababisha mchezo kuvunjwa na mwamuzi baada ya kusubiri kwa dakika 30 bila gari hiyo kutokea.

LIGI DARAJA LA KWANZA
Mechi namba 80 Gipco FC 1 vs Gwambina FC 2- Meneja wa timu ya Gipco Ayubu Msonge amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF) kwa kosa la kumpiga teke mwamuzi wa mchezo huo tajwa baada ya mchezo kumalizika pindi waamuzi walipokuwa wanatoka uwanjani, kitendo hicho kilifanyika February 08, 2020 katika uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita.

– Klabu ya Gipco imetozwa faini ya Tsh 500,000 (laki tano) kutokana na timu hiyo kushindwa kuhakikisha usalama kwenye mchezo uliofanyika February 08, 2020 katika uwanja wa Nyankumbu ikiwa ni jukumu lao kama timu mwenyeji, hivyo kutokea vurugu zilizosababisha kupigwa kwa afisa wa Bodi ya Ligi na waamuzi wa mchezo huo tajwa katika uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43 (1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Uthibiti wa Klabu.

Kamati imeieleza timu ya Gipco FC kuwa endapo vitendo hivyo vitajirudia tena katika mchezo mwingine watakaocheza, haitasita kuchukua maamuzi makubwa zaidi ikiwemo kuwabadilishia uwanja wa nyumbani wa klabu yako (home ground) na kupangiwa uwanja mwingine.

Mechi namba 78- Transit Camp FC 4 vs Mawenzi FC 0– Meneja wa timu ya Mawenzi Fc Christopher Mapunda amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF) kwa kosa la kutolewa kwa kadi nyekundu kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kutoa lugha za matusi katika mchezo huo tajwa uliofanyika February 2, 2020 katika uwanja wa Uhuru jjini Dar es Salaam.