Kauli ya serikali kuhusu wanafunzi waliopo China


Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imewatoa hofu na taharuki Watanzania hususan wazazi, ndugu na jamaa wa wanafunzi takribani 420 walioko katika jimbo la Hubei, mji wa Wuhan Nchini China, ambapo ndio kitovu cha maambukizi ya virusi vya homa ya Corona (COVID-19).


Taarifa ya Wizara imeeleza kuwa hadi sasa hakuna mwanafunzi au Mtanzania yeyote aliyebainika kuambukizwa virusi hivyo na kuwasihi kuendelea kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea kufuatilia hali zao kwa karibu.

 Aidha, Wizara imeeleza kuwa Serikali ya Tanzania haina mpango wa kuwaondoa ama kuwasafirisha wanafunzi hao walioko Wuhan kwa kuwa wako katika uangalizi maalum (quarantine) nchini humo kutokana na serikali kuheshimu masharti na mahitaji ya karantini hiyo yanayozuia mtu yeyote kutoka ama kuingia katika mji huo kwa kusudi la kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo hadi hapo Serikali ya China itakapoondoa karantini hiyo.

'Uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutowaondoa ama kuwasafirisha wanafunzi hao kurejea nyumbani unatokana  na taarifa za kitabibu zinazobainisha kutokea milipuko ya homa ya virusi hivyo katika mataifa ambayo awali yaliwaondoa wananchi wao wakati wa mlipuko na kusababisha kusambaa kwa virusi hivyo na kuleta madhara zaidi kwa mataifa hayo', imeeleza taarifa.

Serikali pia imeesema inakamilisha mpango wa mawasiliano ya moja kwa moja kwa njia za simu (hotline) zitakazotumiwa na wataalamu wa saikolojia (psycho-social support) kwa ajili ya kuwapatia ushauri nasaha wanafunzi na wazazi wakati juhudi za kudhibiti mlipuko huo zikiendelea.

China ilikumbwa na mlipuko wa homa ya corona (the novel coronavirus- 2019-nCoV) ambavyo jina lake rasmi kwa sasa kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni COVID – 19 kuanzia Januari, 2020.