Virusi vya Corona vyagonga hodi Afrika, kisa cha kwanza chathibitishwa Misri


Wizara ya afya ya Misri imetangaza kisa cha kwanza kilichothibitishwa cha mgonjwa wa virusi vya Corona kinachokuwa cha kwanza pia barani Afrika.

Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema mgonjwa aliyebainika siyo raia wa Misri lakini pia haikufafanua uraia wa mtu huyo.

Maafisa wa Misri walifanikiwa kuthibutisha kisa hicho kupitia mpango ulioanzishwa na serikali wa kuwafuatilia abiria waliowasili kutoka nchini ambazo virusi vya Corona tayari vimesambaa.

Msemaji wa wizara ya afya ya Misri, Khaled Megahed, amesema serikali imechukua hatua za tahadhari na inafuatilia kwa karibu afya ya mgonjwa huyo ambayo imeripotiwa kuwa imara.

Mamlaka za Misri pia zimeliarifu shirika la afya duniani WHO kuhusiana na kisa hicho na tangu wakati huo mgonjwa huyo amewekwa karantini katika hospitali maalum ya umma.

Mapema mwezi huu Misri ilifuta safari zote za ndege za shirika la ndege ya taifa kwenda China. Na hatua hiyo itaendelea hadi mwishoni mwa mwezi huu.

Raia 301 na moja wa Misri waliondolewa kutoka mji wa Wuhan, kitovu cha mripuko huo wa virusi nchini China na tangu walipowasili wamewekwa karantini ya siku 14.

Mahusiano ya karibu na China na mifumo dhaifu ya afya ni masuala yanayozua wasiwasi kuhusu uwezo wa nchi za Afrika wa kukabilina na mripuko wa virusi vya Corona vinavyyowauwa maelfu ya watu nchini China.

Hayo yanajiri wakati China imetangaza kuwa maambukizi ya virusi vya Corona yamefikia visa 66,492 huku idadi ya waliokufa imepanda hadi watu 1,523 na wagonjwa wengine 11,053 wako kwenye hali mahututi.

Hata hivyo takwimu zilizotolewa zimeonesha kupungua kwa idadi ya maambukizi mapya ikilinganishwa na zile zilizotolewa siku moja iliyopita.

Lakini kulingana na takwimu hizo idadi ya vifo bado inapanda na katika kipindi cha saa 24 zilizopita vifo vipya 143 vilirikodiwa.

Kwa mara ya kwanza siku ya Ijumaa, China ilitangaza takwimu za maambukizi ya virusi vya Corona kwa wafanyakazi wa afya na kuthibitisha zaidi ya watumishi 1,700 wa hospitali wameambukizwa virusi hivyo.

Virusi vya Coorna vilivyozuka kwenye mji wa Wuhan Disemba iliyopita tayari vimesambaa kwenye mataifa kadhaa ulimwenguni na kusababsiha kitisho kikubwa cha afya duniani.