https://monetag.com/?ref_id=TTIb Kiwanzi na Ukuni kukarabati Barabara | Muungwana BLOG

Kiwanzi na Ukuni kukarabati Barabara



Na Omary Mngindo, Bagamoyo.

Wakazi wa Vitongoji vya Kiwanzi Kata ya Kiwangwa halmashauri ya Chalinze na Ukuni Kata ya Dunda Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wameanza kuchangishana fedha kwa ajili ya kuzikarabati barabara zao.

Hatua hiyo inayolenga kuboresha miundombinu ya barabara hizo, ambazo kwa kipindi kirefu zimechimbika kutokana na mvua, hatua inayosababisha adha kubwa kwa wakazi katika maeneo yao.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiwanzi Miraji Safisha alisema kuwa katika eneo lake mbali ya changamoto ya barabara, pia kuna adha ya baadhi ya wakazi kulima mananasi na kujenga nyumba mpaka ndani ya eneo la barabara, hatua inayoleta adha kwa wengine.

Akizungumza na Waandishi wa habari kitongojini hapo, Miraji alisema kuwa hatua hiyo imetokana na makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano uliofanyika mwishoni mwa mwezi wa pili mwaka huu, ambapo tayari wameshachanga laki tano.

"Katika mkutano huo pia tulifanya harambee ya papo kwa papo, ambapo tulikusanya kiasi cha shilingi laki tano taslimu zikiwemo ahadi za lori za kokoto, mchanga na vifaa mbalimbali vitavyotumika kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizo," alisema Miraji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ukuni Dawson Shigera alisema kwamba wakazi kitongojini hapo wamekubaliana kuchangishana fedha kwa ajili ya kuzifanyia ukarabati barabara zolizopo kwenye eneo lao, ikiwa ni kukabiliana na uharibifu wa miundombinu hiyo.

Aliyasema hayo akizungumza na Mwandishi kwa njia ya simu, ambapo alisema makubaliano hayo yameafikiwa kwenye mkutano uliofanyika mwanzoni mwa mwezi wa pili, ambapo tayari wameshakusanya zaidi ya shilingi laki nane na elfu ishirini.

Alisema kuwa katika Kitongoji chao kina changamoto mbalimbali, ambapo mbali ya barabara kuna majengo yasiyomalizika, yanayotumiwa na watu wanaojihusisha na uharifu, hatua ambayo tayari wameshaifanyiakazi kwa kuwaita wahusika.

Alisema kuwa kuna wakazi wawili kitongojini hapo wamejitolea magari yao mawili makubwa yagayotumika kwa ajili ya kusomba vifusi kutoka maeneo vilivyopo na kuvileta katika maeneo yatayofanyiwa ukarabati huo.

"Katika Kitongoji chetu tuna watu wenye nafasi mbalimbali, mmoja wapo anamiliki greda ambapo amekubali kulitoa bure sisi tuchangie mafuta hatua ambayo tayari tumeshaianza, kama si mvua tungekuwa tumeshaikamilisha hiyo kazi," alisema Shigera.