Mkurugenzi wa wilaya ya Babati atumia mkalimani kufikisha ujumbe wa Corona



Na John Walter-Manyara.

Baada ya serikali kupitia kwa waziri mkuu Kassim Majaliwa kuwataka wananchi kuzingatia matumizi ya Maji tiririka na sabuni,kuepuka Mikusanyiko isiyo ya lazima ili kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Babati Hamisi Malinga katika kufikisha ujumbe huo kwa wanachi ameanza kutoa elimu hiyo kupitia nyumba za ibada.

Katika Kijiji cha Dareda ilimbidi Mkurugenzi huyo kufika katika ibada ya jumapili katika baadhi ya makanisa na kutoa elimu huku akimtumia mkalimani ili na wasioelewa vizuri kiswahili nao waweze kupata ujumbe huo muhimu.

Aidha Malinga aliwataka Wananchi wazingatie ushauri unaotolewa na Serikali na kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Amewaomba viongozi wa dini waendelee kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha waumini wao wote kuzingatia tahadhari za ugonjwa huu unaosambazwa kwa njia ya maji maji kutoka kwa mtu mwenye maambukizi, kusalimiana kwa kushikana mikono au kugusa mahli ambapo muathirika amepagusa.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli jana jumapili machi 22, ametangaza kuwa nchi ina wagonjwa 12 walioambukizwa ugonjwa wa corona, Wanane kati ya wagonjwa hao ni raia wa Tanzania na wengine wanne ni raia wa kigeni.

Ugonjwa huu uliingia hapa nchini mapema mwezi machi baada ya Mtanzania mwanamke mwenye miaka 46 aliyesafiri kwenda nchi za Ubeligiji, Sweden na Denmark hivi karibuni, kupimwa na kuthibitika kuwa na virusi vya Corona (COVID-19).