Yanga yawashtukia Morrison, Tshishimbi dili la Msimbazi

JUZI Alhamisi Machi 19 kulienea tetesi za Simba kutaka kuchomoa baadhi ya vifaa vya Yanga wakiwemo viungo wawili Papy Tshishimbi na Feisal Salum sambamba na kiungo mshambuliaji Bernard Morrison.

Mpango huo ukamfikia Hersi Said, miongoni mwa vigogo wa GSM ambaye jana alianza kupambana na mmoja baada ya mwingine katika kukamilisha kuwabakiza nyota hao.

Mwanaspoti linajua kwamba Bosi huyo ambaye anaaminika zaidi kwa Bilionea wa GSM, Ghalib Mohamed aliifungua rasmi siku ya jana akianza mazungumzo na kiungo Tshishimbi kisha baadaye Morrison akafuata nyuma kwa mpango huohuo.
Hata hivyo, alipotafutwa Hersi alikuwa mgumu kufafanua ingawa Mwanaspoti linafahamu kwamba wakati wowote atamalizana na mastaa hao kwani wameshakubaliana kila kitu.

Mbali na Tshishimbi atalamba miaka miwili, jana alikutana na mkuu huyo akiwa na kocha wake Luc Eymael na baadaye Morrison alitua katika ofisi za bosi huyo huku kikao chao kilikuwa kirefu.

Staa wa mwisho aliyetakiwa kujumuishwa katika mazungumzo hayo alikuwa ni Feisal lakini tayari alishavuka maji akirejea kwao Zanzibar kwa muda mfupi.

Akizungumzia mchakato huo, Hersi alisema; “Tumesikia hayo maneno lakini niseme tu tuko sawasawa, sioni kama kuna mchezaji ambaye klabu inamuhitaji kwa maana ya mapendekezo ya benchi la ufundi halafu akachukuliwa na klabu ya hapa ndani, tupo makini katika hatma ya kila mchezaji ambaye anahitajika hapa, watu watulie kila kitu kinafanyiwa kazi na uongozi wa klabu na sisi GSM.”

Yanga wamepania kuwadhibiti mastaa wao wote wa maana lakini wamempa jeuri kocha kusajili sehemu yoyote anayotaka kwani wanataka msimu ujao kuja na nguvu mpya na kila kitu wanataka kumaliza mapema kabla kwenye usajili hapajakucha.