Baada ya mbunge kukosa hewa wakati anachangia, Spika awatahadharisha wabunge "makombora ni mengi kuelekea uchaguzi kuweni makini"

WAKATI Bunge likielekea ukingoni na wabunge kurudi tena kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu 2020, Spika wa Bunge Job Ndugai amewashauuri wabunge hao kuwa makini kwani makombora ni mengi kipindi hiki.

Akizungumza leo Bungeni Mjini Dodoma Spika Ndugai amewaambia wabunge kuwa hiki ni kipindi ambacho wanatakiwa kuwa makini wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu makombora jimboni yanakuwa mengi, hivyo wachukue tahadhari.

Ushauri huo wa Spika Ndugai kwa wabunge umekuja baada ya Mbunge Anastazia Wambura kushindwa kuendelea kuchangia Bungeni baada ya kueleza kuwa anakosa hewa na sauti inakauka."Mheshimiwa Spika naona nakosa hewa,"alikuwa akisikika mbunge huyo .Hata hivyo aliomba kuunga mkono hoja na kukaa kwenye kiti chake.

Baada ya kutoa maelezo hayo ,Spika Ndugai ndipo aliposikika akiwaambia wabunge wawe makini maana dakika zenyewe hizi ni za kuelekea uchaguzi mkuu , hivyo makombora ni mengi."Tena na hivi kuna Corona unaweza kukutana na kombora halafu wakasema Corona. Watani zangu wanyamwezi wanajua namna ya kujifusha ule moshi kwa kujifunika shuka, tuwe makini."