Makonda amuandikia barua Jafo kuingilia kati mabasi ya mwendokasi



Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam imemuandika barua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Seleman Jafo aangalie uwezekano wa kuyaruhusu mabasi 200 ya mwendokasi yaliyokwama kwenye bandari kavu ya Ubungo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Aprili Mosi, 2020 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati akizungumza na wananchi wa mkoa huo  katika kituo cha daladala cha Makumbusho, kuhusu changamoto za usafiri hasa katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya  corona.

“Suala la mwendokasi halipo chini ya mamlaka yangu, lazima wana Dar es Salaam mfahamu bali lipo chini ya Tamisemi. Hivi tunavyoongea watu wangu wanamaliza kuandika barua.

“Nimemuomba Jafo aingilie kati, ninafahamu yapo mabasi si chini ya 200 ya mwendokasi yameegeshwa  pale Ubungo bandari kavu. Nafahamu kuna mgogoro lakini kwa hali tuliyo nayo sasa hivi, nimemuandikia barua kuyaruhusu magari yale yaingiea kwenye mfumo ili wakazi wa Kimara wasirundikane na kubanana,” amesema Makonda.

Huku akitoa tahadhari ya mara kwa mara kuhusu virusi vya corona  katika mkutano huo, Makonda amesema hatua hiyo itasaidia wakazi wa maeneo ya Ubungo, Kimara na Mbezi kuwahi kazini.