Mfahamu mwanamziki John legend

Desemba 28, 1978 alizaliwa mwanamuziki, miwmbaji, mtunzi wa nyimbo, prodyuza, mwigizaji wa Marekani maarufu kwa jina la John Legend.

Jina lake halisi ni John Roger Stephens. Alizaliwa Springfield jimboni Ohio. Ni miongoni mwa watoto wanne wa Mzee Llyod Elaine na Romar Lamar Stephens.

Baba yake alikuwa ni mfanyakazi wa Viwandani. Mzee Lyod alikuwa mpiga wa ngoma kanisani wakati mama yake alikuwa mwimbaji na kiongozi wa kwaya huku bibi yake alikuwa mpigaji wa vyombo vya muziki.

Ikiwa na maana kwamba John Legend ametokea katika uzao wa wanamuziki. Mnamo mwaka 2004 Legend alikaririwa akisema wazazi wake waliachana kwa miaka 12 kabla ya kurudiana tena.

Legend alifundishwa kusoma na mama yake akiwa nyumbani. Akiwa na miaka minne alikuwa akiimba na kwaya kanisani. Alianza kupiga kinanda akiwa  na miaka saba.

Kutokana na kuwa na uwezo mkubwa darasani alirushwa madarasa mawili. Akiwa na umri wa miaka 12 Legend aliingia katika shule ya sekondari ya Springfield North ambako alihitimu akiwa na ufaulu mzuri akishinda nafasi ya pili.

Kwa maelezo yake mwenyewe Legend alisema alipata ofa kutoka Chuo Kikuu cha Havard lakini alipata ufadhili kutoka Chuo Kikuu cha Georgetown na Chuo cha Morehouse.

Alienda pia kuchukua masomo ya Lugha na Utamaduni hususani African American Literature na Kiingereza. Akiwa Chuo Kikuu alikuwa Rais na mkurugenzi wa bendi na kundi la Capella lililofahamika kwa jina la Counterparts.

Katika uimbaji wake aliachia ya kwanza mnamo mwaka 2004 aliyoipa jina la Get Lifted. Pia ameshirikishwa katika nyimbo mbalimbali na wasanii kama Kanye West, Jay Z na Alicia Keys. Wimbo wa All of Me ulikuwa katika albamu ya nne ya Love in the Future (2013).


Wimbo huo ulimweka kukaa katika Billboard Hot 100 ukiwa katika nafasi ya kwanza. Mnamo mwaka 2007 Legend alipokea tuzo ya Hal David Starlight kutoka Songwriters Hall of Fame. Pia alishinda tuzo ya Academy na Golden Globe mnamo mwaka 2015. Pia ameshinda tuzo 10 za Grammy.

Mnamo mwaka 2017 alitunukiwa tuzo ya Tony kwa kufanya kazi na Jitney. Pia aliwahi kushiriki tuzo ya Primetime Emmy na kushinda katika kipengele cha prodyuza bora wa kipindi akiwa ni miongoni mwa watu weusi 15 waliowahi kutwaa tuzo Emmy, Grammy, Oscar na Tony (EGOT).



Legend anakuwa mtu wa pili mwenye umri mdogo kupata mafanikio makubwa.