Mgonjwa wa Corona Akikohoa Anasambaza Virusi 3,000

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu ya covid-19 vina uwezo wa kukaa kwenye nguo kwa saa 12 huku anayekohoa mara moja akisambaza virusi 3,000.

Ofisa Programu wa elimu ya afya kwa umma kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Tumaini Haonga alisema kuwa hiyo inamanisha iwapo mtu mwenye mambukizi ya virusi vya corona akapiga chafya na ikatua kwenye nguo ya mtu, au kitambaa chochote kama pazia za madirisha au milango, au makochi ya vitambaa na mtu mwingine akashika basi atapata mambukizi ya ugonjwa huo, iwapo havijasafishwa stahiki.

Dk Haonga alisema: “Hakuna ushahidi rasmi wa kisayansi kwa muda ambao virusi vinatumia kukaa hewani, lakini kwenye maeneo kama uso, nguo au maeneo yenye unyevunyevu kwa utafiti wa sasa hivi umeonesha kuwa vinaweza kuendelea kuwa hai kwa muda wa saa tisa hadi 12,” alisema.

Alisema hiyo imetokana na tafiti za watalamu wa afya duniani ambapo inaelezwa kuwa mtu akikohoa mara moja tu, anaweza kusambaza virusi 3,000. Kama ilivyo katika maambukizi ya kupumua mafua yakiwemo, maambukizi ya virusi vya corona yanaweza kusambaa pale ambapo mtu akikohoa na vijidudu vikabaki kwenye mkono na akashika kwenye pua na mdomo.

Hata hivyo kwa mujibu wa watalamu wengine ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO)ni kwamba kuna uwezekano kirusi hicho cha corona kukaa hewani kwa dakika 45. Baadhi ya wataalamu hao husema kikohozi cha kawaida ambacho hakina maambukizi, kina udogo wa mara 30 ya unywele wa binadamu, kina uwezo wa kubaki hewani kwa dakika hizo 45.

Kutokana na hali hiyo, Dk Haonga alisema ili kujikinga na ugonjwa huo wa covid-19 ni kuhakikisha unavaa barakoa unapolazimika kuwa maeneo ya mikusanyiko, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono na maji tiririka na sabuni mara nyingi zaidi, epuka kushika uso, pua na macho kwani tafiti zinaonesha binadamu anashika uso mara 45 kwa siku.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items