Mkutano wa OPEC+ waahirishwa kufuatia mzozo kati ya Saudi Arabia na Moscow


Jumuiya ya nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC na Urusi wameahirisha mkutano uliokuwa ufanyike kesho Jumatatu kujadili kupunguza uzalishaji wa mafuta.

Mkutano huo sasa utafanyika tarehe 9 Aprili. Tamko hilo limetolewa wakati mzozo kati ya Urusi na Saudi Arabia kuhusu nani wa kulaumiwa kufuatia kuongezeka kuporomoka kwa bei ya mafuta ghafi.

Hatua ya kuchelewesha mkutano huo imekuja baada ya shinikizo kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump kwa jumuiya hiyo ya nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani inayoongozwa na Saudi Arabia na washirika wake, kurejesha utulivu katika masoko ya mafuta duniani mara moja.

Bei ya mafuta ilishuka kabisa kuanzia Machi 30 kutokana na kupungua kwa mahitaji ya bidhaa hiyo kufuatia kusitishwa kwa shughuli za kila siku ili kudhibiti mripuko wa virusi vya corona unaoendelea kuihangaisha dunia.