Ufaransa, Uhispania zaongeza idadi ya waliokufa kwa corona


Ufaransa imeripoti kiwango kikubwa zaidi cha vifo vinavyotokana na kirusi cha corona, ambapo watu 499 walipoteza maisha yao kwa siku ya jana pekee, na kuifanya idadi kamili nchi nzima kufikia 3,523.

 Waziri wa Afya Jerome Salomon, anasema kwa sasa watu 22,757 wamelazwa hospitali ambapo 5,565 kati yao wako kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi.

Hata hivyo, takwimu hizi za Ufaransa zinajumuisha wale tu waliofia hospitalini na sio wanaofia majumbani mwao au kwenye nyumba za kutunza wazee.

Idadi jumla ya watu walioambukizwa imechupa kwa 7,578 na hivyo kufikia 52,128 hadi jana, Jumanne.

Nchini Uhispania, vifo 849 vimeripotiwa ndani ya masaa 24 yaliyopita, ikiwa ni siku ya nne mfululizo kwa idadi ya vifo kupindukia 800 kwenye taifa hilo, ambalo limethibitisha maambukizi mapya 9,000 ndani ya siku moja, na kuifanya idadi ya walioambukizwa kukaribia 100,000.

Hadi sasa, watu 8,189 wameshapoteza maisha yao.