Waziri wa sheria na usalama nchini Brazil Sergio Moro amejiuzulu baada ya kuzozana na Rais Jair Bolsonaro kuhusu kufutwa kazi kwa mkuu wa jeshi la polisi.
Moro, ambaye ni jaji wa zamani wa mahakama ya kupambana na ufisadi, alitaja kile alichosema ni uingiliaji wa kisiasa katika polisi ya taifa, akisema hawezi kufanya kazi yake bila uhuru wa idara ya polisi.
Bolsonaro alimshambulia Moro, akimtuhumu kwa kuwa na kiburi na kutoa tuhuma zisizo za msingi. Rais huyo alidai kuwa aliwaambia wabunge kadhaa kabla ya Moro kutangaza kujiuzulu kwake, kwamba watamuona mtu ambaye anajithamini mwenyewe kuliko kujitolea kwa ajili ya Brazil.
Hatua ya Moro imekuja baada ya Bolsonaro kumfuta kazi mkuu wa polisi Mauricio Valeixo, ambaye ni mshirika wa karibu wa Moro.
Bolsonaro alisema alimuondoa Valeixio kwa sababu alitaka mtu ambaye angeweza kuwa na mawasiliano ya kibinafsi, kumpigia simu, kumuuliza habari, na ripoti za kijasusi.
