Wimbi la pili la nzige linatarajiwa kusababisha uharibifu mkubwa mashariki mwa Afrika, miezi miwili baada ya kundi la wadudu hao hatari kuvamia mimea muda mfupi tu kabla ya kuanza kwa mlipuko wa virusi vya corona.
''Inaonekana kwamba wale waliokwepa Covid 19 watakabiliana na Locust 19'', alisema Akiwumi Adesina rais wa benki ya maendeleo barani Afrika na waziri wa zamani wa kilimo.
Nzige tayari wamevamia nchini Somalia, Ethiopia, Kenya, Uganda, Ethiopia na Sudan Kusini mara moja mwaka huu, mwezi Januari na Februari.
''Sasa makundi hayo ya nzige baada ya kuzaa mayai ,yanaweza kuwa mara 20 zaidi ya yalivyokuwa'', amesema mtaalam huyo.
''Mara ya mwisho Kenya kuathiriwa na uvamizi wa nzige wa kiwango kama hiki ni miaka 70 iliopita wakati ilipokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza', alisema Keith Cressma, mtaalamu wa utabiri wa nzige katika shirika la chakula na kilimo katika Umoja wa mataifa FAO.
Uvamizi huo unahatarisha kusababisha tatizo la chakula ambalo tayari limekuwa likitarajiwa katika upembe wa Afrika.
Asilimia 40 ya watu milioni 160 katika eneo hili hawapati lishe bora, kulingana na FAO.
