Burundi itafanya uchaguzi Jumatano ijayo, unatarajiwa kumaliza uongozi wa Rais Pierre Nkurunziza wa miaka 15.
Wakati Nkurunziza atakapokabidhi madaraka, itakuwa ni kwa mara ya kwanza taifa hilo la Afrika Mashariki linabadilisha uongozi kwa njia ya amani tangu ilipopata uhuru mnamo mwaka 1962.
Lakini janga la virusi vya corona linaibuwa wasiwasi wakati wa uchaguzi huo utakaofanyika Mei 20. Aidha Burundi imewafukuza nchini mwake wafanyakazi wa Shirika la Afya Duniani WHO, baada ya shirika hilo kueleza wasiwasi wake.
Serikali imekuwa ikishutumiwa kwa kutoa idadi zisizo za kweli za maambukizi hayo. Halikadhalika Burundi inaonekana kutumia hatua za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona kuzuia idadi ya waangalizi wakigeni wa uchaguzi kuingia nchini humo, kwa kuonya kwamba kuanzia Mei 8 kila mgeni atakaeingia nchini humo atawekwa karantini kwa muda wa siku 14.
