Hospitali ya Rufaa Manyara yaomba Msaada wa Vifaa Kinga vya Corona


Na John Walter-Manyara
Madaktari na wahudumu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara wameomba wahisani, wafadhili na watu mbalimbali kuwasaidia vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona.
Wametoa ombi hilo wakati wakipokea msaada wa vitakasa mikono  vifaa vilivyotolewa na Shirika la kuhudumia Viwanda (SIDO) Mkoa wa Manyara.
Akizungumza kwa niaba ya mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Daktari wa Magonjwa ya ndani Dr. Yesige Mutwajaa,  alisema kwa sasa wana uhaba wa vifaa Kinga hivyo kwa mtu yeyote,kampuni au Taasisi iwasaidie kupata vifaa vitakavyoweza kuwasaidia kwenye mazingira yao ya kazi.
Dr. Yesige  alisema kuwa serikali peke yake haitaweza kufanya kila kitu hivyo wadau wanapojitokeza kusaidia vifaa kinga itarahisisha mapambano na kuvishinda virusi vya corona kwa pamoja.                               
Meneja wa SIDO Mkoa wa Manyara Abel Mapunda akikabidhi vifaa hivyo, amesema wameamua kutoa msaada wa vifaa hivyo ili viweze kuwasaida wataalamu wa afya na wahudumu katika hospitali hiyo katika  kuwasaidia kujikinga na ugonjwa huo ikizingatiwa kuwa wanawahudumia wagonjwa wengi wakiwemo wa Corona.
Mapunda alisema kuwa utoaji wa msaada huo ni  katika jitihada za kuendelea kukabiliana na ugonjwa wa homa ya Mapafu-Corona.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items