Magufuli amaliza kero ya tatizo la gari la wagonjwa


     Na Hamisi Abdulrahmani, Masasi

  WANANCHI wa kata ya Nagaga Halmashauri ya wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara wamempongeza raisi Dk.John Pombe Magufuli kwa kuwapatia Gari la kubebea wagonjwa(Ambulance) lenye thamani ya zaidi ya sh.120 milioni kwa ajili ya kumaliza tatizo la ukosefu wa Gari la kubeba wagonjwa kwenye kituo cha afya cha Nagaga kilichopo wilayani humo.

  Gari hilo la kubebea wagonjwa limekabidhiwa jana mbele ya viongozi mbalimbali wa serikali na kisiasa ambapo mkuu wa wilaya ya Masasi,Selemani Mzee ndiye aliyekabidhi Gari hilo kwa uongozi wa kituo cha afya cha Nagaga kwa niaba ya raisi Dk.John Magufuli.

   Akizungumza kabla ya kukabidhi Gari hilo Mkuu wa wilaya huyo,Selemani Mzee alisema Gari hilo limetolewa na raisi Dk.Magufuli ikiwa ni ahadi yake ambayo aliitoa mapema mwaka huu alipofanya ziara wilayani Masasi baada ya kupokea kero hiyo ya kituo cha afya cha Nagaga kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Gari la kubebea wagonjwa(Ambulance)

   Alisema raisi Dk.Magufuli ameamua kutekeleza ahadi yake hiyo baada ya kuguswa na adha ya wananchi wa kata hiyo ambao wanapata huduma za afya katika kituo cha afya cha Nagaga 

  Mzee alisema kwa muda mrefu wananchi wa kata ya Nagaga wanaopata huduma ya afya katika kituo cha afya cha Nagaga wamekuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa Gari la wagonjwa hivyo uwepo kwa Gari hilo kwa sasa kutasaidia kuondoa adha hiyo.

  “Raisi ametoa Gari hili baada ya kusikia kilio chenu kupitia Mbunge wenu wa jimbo la Lulindi na lengo lake raisi ni kuona wananchi wake hawapati changamoto zozote kwenye sekta ya afya hivyo maagizo yake Gari hili mlitunze ili liwasaidie,”alisema Mzee

  Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi,Changwa Mkwazu ameiopongeza serikali na raisi Dk.Magufuli kwa kutoa Gari hilo ambalo ni wazi kabisa limekuja kumaliza kero ya muda mrefu ya ukosefu wa Gari la wagonjwa katika kituo cha afya cha Nagaga.

  Mkwazu alisema licha ya raisi Dk.Magufuli kutoa msaada huo wa Gari kwa kituo hicho cha afya cha Nagaga lakini serikali yake imekuwa msatari wa mbele kutoa fedha mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maedneleo inayowalenga wananchi mojo kwa moja.

  “Mimi namshukuru raisi Dk.Magufuli kwanza kwa kutoa msaada huu wa Gari la wagonjwa kituo cha afya Nagaga lakini pia fedha zingine zinazoletwa katika Halmashauri yangu kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo zile za ujenzi wa hospitali ya wilaya inayojengwa katika kijiji cha Mbuyuni kwa thamani ya sh.1.5 bilioni,”alisema Mkwazu

  Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake wa kata hiyo ya Nagaga, Fatuma Abdallah alisema yeye kwa niaba ya wanawake na wananchi wote kwa ujumla wanampongeza raisi Dk.Magufuli kwa kusikia kilio chao cha ukosefu wa Gari la wagonjwa katika kituo cha afya cha Nagaga

   Alisema awali wananchi hao walikuwa wakitumia vyombo mbalimbali kuwabeba wagonjwa kuwapeleka kupata huduma za afya kama vile baiskeli,pikipiki na bajaji tena kwa gharama kubwa lakini sasa unafuu umepatikana baada ya raisi Dk.Magufuli kutoa Gari hilo.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items