Mbowe: Corona haihitaji kiburi

FREEMAN Mbowe, Mwenyikiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema mapamba ya ugonjwa wa corona hayahitaji mdhaha wala kiburi.

Akizungumza na wananchi kupitia mitandao ya kijamii leo tarehe 17 Mei 2020, amesema Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi kwa siku mbili (9-10 Mei), imeweka tofauti za kisiasa pembeni katika vita dhidi ya virusi vya corona.

“….janga hili halihitaji masihara, halihitaji mdhaha wala halihitaji usiri katika kulikabili. Ilitambua (Kamati Kuu) kuweka tofauti zetu pembeni, na kutoruhusu chuki za kisiasa, kiburi cha madaraka na mamlaka ya kupambana na vita hii ya corona.”

Amesema, kutokana na ripoti mbalimbali za kimataifa na tafiti za kisayansi, janga la corona sio jambo la kuisha haraka na kwamba, ni janga ambalo taifa inapaswa kujipanga kuishi nalo kwa muda mrefu.

Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Kilimanjaro amesema “hakuna njia ya mkato, ni lazima taifa kufikiria kwa mawanda mapana katika kulikabili janga hili.”

Amewataka Watanzania kutambua kuwa, ugonjwa huo utakuwa na athari kubwa katika maeneo mbalimbali ya uchumi kwa muda mrefu.