Netanyahu: Mashtaka dhidi yangu ni njama ya kunopindua

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amevishambulia vikali vyombo vya sheria vya nchi yake, akivituhumu kula njama ya kumuondoa madarakani, na kujitaja kuwa kiongozi imara wa sera za mrengo wa kulia.

Netanyahu alisema hayo jana alipofikishwa mahakamani, katika kesi iliyokuwa ikisubiriwa kwa shauku kubwa. Amekuwa akiandamwa na shutuma za ufisadi kwa muda wa miaka mitatu, na kesi hiyo iliahirishwa mwezi Machi kutokana na janga la corona.

 Netanyahu amekuwa Waziri Mkuu wa kwanza aliyeko madarakani kufikishwa mahakamani tangu kuundwa kwa taifa la Israel zaidi ya miaka 70 iliyopita.

 Kiongozi huyo ameishutumu polisi, waendesha mashtaka, vyombo vya habari na mfumo mzima wa sheria, kufanya hila ya kumpindua kinyume na matakwa ya wananchi.

Wakosoaji wake wamesema kauli yake ya kuvikosoa vyombo vya sheria inaweza kuathiri imani ya wananchi juu ya vyombo hivyo.