Promota: Tutapoteza Mabondia Wengi

PROMOTA wa ngumi za kulipwa, Ally Mwanzoa, amesema kuna hatari ya kuwapoteza mabondia wengi kutokana na kukosa fedha za kujikimu kila siku kwa sababu hakuna wanachoingiza kwa sasa kufuatia kuwapo wa virusi vya corona.

Mwanzoa aliliambia gazeti hili jana kuwa, kipindi hiki mambo mengi yamesimama na mabondia wengi hutegemea kucheza mapambano kama ajira, hivyo kukaa muda mrefu bila kucheza itawakatisha tamaa na kukimbia kutafuta kwingine.

“Kipindi hiki ambacho tuko nyumbani mabondia wanaathirika ukitegemea hakuna mapambano ya ndani na nje, tatizo hili kama litakaa kwa muda mrefu wengi watakimbia kwenda kutafuta kazi nyingine zitakazowaingizia kipato,” alisema.

Alisema hakuna kinachofanyika katika kila sekta ya ngumi, mambo yamekuwa hayaendi vizuri hata kamisheni ya ngumi hakuna inachofanya labda hadi michezo itakaporejeshwa na haiwezi kuwa kwa mara moja ni lazima itachukua muda watu kuwa sawa.

“Mabondia hawapati nafasi ya kufanya mazoezi kwa nafasi na uhuru kwa kuhofia kupata maambukizi ya virusi vya corona, kitendo ambacho kinaweza kupoteza ufanisi wao pindi watakaporejea baadaye,” alisema.

Alisema wanaendelea kusubiri hadi Juni kuona kama serikali itarejesha michezo kama alivyosema Rais John Magufuli, lakini wanafikiria kuandaa mapambano ya ndani ili kurudisha viwango vya mabondia kabla ya kushiriki ya kimataifa baadaye.

“Mpaka corona iishe mabondia watashuka viwango, hatutegemei kuwaona katika ufanisi, itawachukua muda kukaa vizuri na kurudi kucheza mapambano ya kimataifa, tumeona kama michezo itarudi mabondia wapambane wenyewe kwa wenyewe kwanza kujiimarisha ,” alisema.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items