Sikonge yaagiza ianze kutibu wananchi katika hospitali ya wilaya yake


IDARA ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imeagizwa kuhamia katika jengo la Utawala katika Hospitali ya Wilaya hiyo na waanze kutoa huduma ya watibabu kwa wananchi.

Kauli hiyo imeolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri wakati akitoa salamu za Serikali katika Kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu

Alisema wakati wakiendelea kusubiri vifaa tiba na vifaa vingine kwa ajili ya Hospitali hiyo ya Wilaya ni vema wakaanza na utoaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa nje.

Magiri aliutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge kutoa walau sehemu ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kujenga vyoo ili majengo yote muhimu ya awali yawepo na huduma zianze.

Alisema wanaweza kuanza kutoa huduma kama zile zinazotolewa kwa kiwango cha Zahanati cha kuanzia walau asubuhi hadi jioni kila siku.

Magiri alisema hatua hiyo itawasaidia wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo wasipate shida ya kuembea umbali mrefu kutafuta huduma kupima malaria na magonjwa mengine.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Peter Nzalalila alisema majengo ya Hospitali ya Wilaya hiyo hayakujengwa kutazamwa bali kutoa huduma kwa wananchi.

Alisema ni vema Mejimenti ya Halmashauri hiyo ikaangalia uwezekano wa kuanza kutoa huduma za matatibu katika eneo hilo kwa kutumia watalaamu waliopo wakati wakisubiri kupata wengine.