Taasisi ya GFF yamkabidhi vifaa va kujikinga na corona DC Mpwapwa


TAASISI ya Glaring Future (GFF) imekubali kushirikiana na serikali katika kuelimisha wanafunzi madhara ya mimba katika umri mdogo, matumizi ya dawa za kulevya na elimu ya kujitambua pamoja na kupeleka vipima joto kwa ajili ya kupimia maambukizi ya ugonjwa wa Corona pindi wanafunzi watakaporejea mashuleni.

Ahadi hiyo imetolewa wilayani Mpwapwa na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo , Jabir Shekimweri wakati walipomtembelea ofisini kwake na kumkabidhi vifaa mbalimbali vya kujikinga na Corona ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Vifaa ambavyo GFF imekabidhi ni Ndoo 30 za Lita 20 kwa ajili ya kunawia mikono na maji tiririka, Vitakasa Mikono 12 vya Mililita 500, Sabuni za kunawia mikono 25 pamoja Vikinga Uso (Face shields) 30 ambazo vyote kwa pamoja vina thamani ya Sh Milioni Moja.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri ameipongeza taasisi hiyo kwa kuungana na serikali katika kipindi hiki lakini pia kwa kuchagua Wilaya hiyo huku pia akiwaomba wadau wengine kujitokeza.

" Niwapongeze na niwashukuru sana, huu ni Moyo wa ajabu sana ambao kwa hakika Mwenyezi Mungu atawalipia. Niwasihi tuendelee kushirikiana kwa pamoja katika kuwahudumia watanzania wenzetu, na mimi niwaambie tu niko tayari kuwapa sapoti yoyote katika jambo lolote la kimaendeleo ambalo mtaguswa nalo wilayani kwetu.

Niwaombe pia katika kipindi hiki ambacho taasisi zingine kama Shule ya Sekondari zinafunguliwa tunaomba ikiwapendeza pia mtuletee na vipama joto  kwa ajili ya kupimia joto wanafunzi wetu, lakini mrudi tena kutoa elimu ya kujitambua kwa wanafunzi hasa watoto wa kike," Amesema DC Shekimweri.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi hiyo ya GFF, Aisha Msantu amempongeza Rais Dk John Magufuli kwa namna ambavyo amechukua hatua madhubuti za kupambana na ugonjwa huo nchini kwa kuangalia mazingira ya Nchi yetu bila kufuata presha ya Mataifa menginge.

Amesema wataendelea kushirikiana na serikali katika kuwahudumia watanzania huku akiahidi kurudi tena wilayani hapo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi lakini pia kuwapa elimu ya ujasiriamali vijana wa Mpwapwa.

" Tukushukuru Mhe DC kwa kutupokea, sisi tunaguswa na kasi ya serikali yetu chini ya Rais Dk Magufuli kwa namna inavyotuhudumia wananchi wake, tunaahidi huu hautokua mwisho wetu sisi kuja hapa Mpwapwa tutaendelea kuja kwa ajili ya kusaidiana na watanzania wenzetu kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu na Ujasiriamali," Amesema Msantu.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items