WHO: Amerika Kusini imekuwa kitovu kipya cha janga la corona

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema Ijumaa kwamba Amerika Kusini imekuwa kitovu kipya cha janga la virusi vya corona, huku idadi ya maambukizi pia ikiongezeka katika baadhi ya mataifa ya Afrika.

 
Mkuu wa kukabiliana na matukio ya dharura wa WHO, Mike Ryan amesema Brazil ndiyo nchi iliyoathirika zaidi Amerika Kusini, na kwamba imeizidi Urusi na kuwa nchi ya pili yenye idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona baada ya Marekani. Data zilizokusanywa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, zimedhihirisha kwamba Urusi hadi hivi sasa imerikodi maambukizi yapatayo 326,448  ya ugonjwa wa COVID-19. Na, hadi kufikia Ijumaa jioni, Marekani imeripoti maambukizi yanayopindukia milioni 1.6.

Siku ya Ijumaa kumeripotiwa maambikizi mapya 20,803, na kuifanya idadi jumla Brazil kuwa 330,890 kulingana na Wizara ya Afya nchini humo. Watu wapatao 21,048 wamefariki, ikiwa ni idadi ya sita ya juu ya vifo ulimwenguni kote, kulingana na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.


Kwa upande wa Afrika, shirika hilo limesema maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 yaliyothibitishwa hadi sasa yanapindukia 100,000 barani humo. Ryan amesema katika wiki iliyopita, nchi tisa za Afrika zimerekodi asilimia 50 ya ongezeko la maambukizi hayo, wakati mataifa mengine barani humo yanashuhudia kupungua kwa idadi ya maambukizi.


Wakati huo huo Rais wa nchi hiyo Donald Trump amesema kwamba amewatolea wito magavana kufungua tena nyumba zote za ibada wikiendi hii, licha ya kitisho cha kuenea kwa virusi vya corona.

Trump amesema nyumba za ibada ikiwa ni pamoja na makanisa, masinagogi na misikiti ni maeneo yanayotoa huduma muhimu kwa jamii. Aidha amesema ikiwa magavana hao hawatotimiza ombi lake, basi atachukua hatua mikononi mwake, ingawa haijulikani wazi ana mamlaka gani ya kufanya hivyo.

Wakristo wa kihafidhina ni kundi muhimu la wapiga kura, ambalo Trump analihitaji kumpigia kura ili acahguliwe tena kwa muhula mwengine wa urais katika uchaguzi ujao mnamo mwezi Novemba.

Kwengineko Mashariki ya Kati, virusi vya corona vinaaminika kusambaa kote nchini Yemen, ambako mfumo wa afya umesambaratika, huku Umoja wa Mataifa ukitoa wito wa ufadhili wa haraka kupambana na hali hiyo.

Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA), amesema wafanyakazi wa kutoa misaada wanashindwa kuwapatia huduma ipasavyo raia wa Yemen kwa sababu hawana oksijini ya kutosha au vifaa vya kutosha vya kinga dhidi ya virusi hivyo.

Shirika la madaktari wasio na mipaka MSF limesema kituo kikuu cha kutoa matibabu ya virusi vya corona kusini mwa Yemen kimerikodi vifo vya watu wasiopungua 68 katika kipindi cha wiki mbili zilizopita. Umoja wa Mataifa unakadiria utahitaji dola bilioni mbili ili kushughulikia miradi ya misaada nchini Yemen hadi mwisho wa mwaka.

Na barani Asia,  China haikurekodi maambukizi mapya ya ugonjwa wa COVID-19 Mei 22, ikiwa ni mara ya kwanza ya kutoongezeka kwa idadi ya maambukizi tangu janga hilo lilipoanza katika mji wa Wuhan mwishoni mwa mwaka jana.