China na Iran zaikosoa Marekani kuhusu haki za binadamu

China na Iran ambazo kwa miaka iliyopita zimetajwa kama nchi za kiimla na zinazotawaliwa kwa mtindo wa mabavu na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, zimeitaka Marekani katika siku za karibuni kushughulikia suala la ubaguzi na kulinda haki za waliowachache nchini humo.

Vurugu za nchini Marekani kufuatia kifo cha Mmarekani mweusi kilichotokea mikononi mwa polisi zimeugeuza mkondo wa kawaida wa kidiplomasia kuhusiana na suala la haki za binadamu wakati nchi zilizoandamwa na ukosoaji wa Marekani katika kipindi cha miaka kadhaa sasa zimeigeukia nchi hiyo na kuwashutumu maafisa wa Marekani kwa undumilakuwili.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Hua Chunying ametumia maneno ya kauli ya mwisho iliyotolewa na George Floyd Mmarekani mweusi aliyeuwawa akisema,siwezi kupumua,katika ujumbe wa Twitta kumjibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Morgan Ortagus aliyeikosoa hatua ya China ya kuweka sheria za kiusalama kwa raia wa HongKong.