DC Ikungi mkoani Singida azindua mnada mkubwa wa mifugo na mazao

HALMASHAURI ya Wilaya ya Ikungi imezindua mnada wa mifugo na mazao katika Kijiji cha Ighuka kwa ajili ya kutengeneza soko kwa wafugaji na wakulima.

Akizungumza juzi kwenye uzinduzi wa mnada huo mgeni rasmi wa hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo alisema mnada huo ni wa muhimu sana katika wilaya hiyo.

Alisema katika wilaya hiyo hususani Kata ya Ikungi ina zaidi ya kata 10 ambazo zinazunguka eneo hilo na kuwa zina ng’ombe wasio pungua 80,000 na mbuzi 55,000.

“Mifugo hiyo yote pamoja na mazao inahitaji soko hivyo tumeona tufungue soko kwa ajili ya kuuza mifugo hiyo lakini pia tuna ndugu zetu na wazazi wetu ambao wanafanya shughuli za kilimo hivyo wapate sehemu za kuuza bidhaa zao” alisema Mpogolo.


Alisema mnada huo utawakutanisha wauzaji na wanunuzi na utasaidia kuongeza kipato cha wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo na halmashauri itapata fedha baada ya mifugo itakayo uzwa kulipiwa kodi.

Mpogolo alisema katika eneo hilo waliona kulikuwa na mahitaji ya watu wakitaka kununua kuku, mbuzi na mahitaji mengine hivyo ilikuwepo changamoto ya kuwakutanisha ndio maana wakaamua kuanzisha mnada huo.

Alisema mtu anayependa kuuza mifugo na mazao eneo ambalo linaushindani wa wanunuzi bei inapanda, wao kama Serikali waliona ni vizuri wawatafutie soko pia kuwatangazia fursa watakayoipata kupitia mnada huo.

Alisema mnada huo utatoa fursa kwa wauza vyombo vya nyumbani, vinywaji mbalimbali, wapika chakula, nguo na vitu vingine vingi kupata wateja kwa urahisi tofauti na ilivyokuwa hapo awali.


“Zamani katika mnada huu walikuwa wakichinja ng’ombe mmoja kwa ajili ya kitoweo lakini leo hii wamechinja ng’ombe sita na mbuzi 11 ambao wamekwisha na wamekwenda kuongeza wengine wakati mwanzo walikuwa wakichinja mbuzi kati ya watatu hadi sita tu” alisema Mpogolo.

Mfanyabiashara wa nyama choma katika eneo hilo James Yesaya aliwashukuru viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kuanzisha mnada huo ambao unafaida kubwa kwao na akawaomba wautangaze ili watu waujue na waweze kufika kununua mahitaji mbalimbali.

Katika hafla ya kuzindua mnada huo wananchi na viongozi mbalimbali walioudhuria waliwapongeza viongozi wa halmashauri hiyo kwa kuwa wabunifu na kufanikiwa kuanzisha chanzo hicho cha mapato.