Makamu wa Rais wa Marekani afuta mikutano ya kampeni kutokana na COVID-19

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence ametangaza kufuta mikutano ya kampeni katika majimbo mawili ya Florida na Arizona iliyopangwa kufanyika wiki inayokuja baada ya majimbo hayo kushuhudia wimbi la visa vipya vya maambukizi ya virusi vya corona.

Pence alipangiwa kuwa na mkutano wa kampeni mjini Tuscan, Arizona siku ya Jumanne kabla ya kwenda Florida siku ya Alhamisi kwa mkutano mwingine kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba.

Akizungumza akiwa mjini Washington, Pence amesema amefuta ratiba hiyo na badala yake atayatembelea majimbo hayo mawili pamoja na Texas kupata taarifa za kina juu ya kuongezeka kwa visa vya ugonjwa wa COVID-19 kwenye maeneo hayo.

Magavana wa majimbo hayo matatu wanakabiliwa na ukosoaji mkubwa wa kuendelea na mipango ya kufungua tena shughuli za kawaida licha ya kuongeza kwa visa vya maambukizi kwenye maeneo hayo.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items