Jibu la Zarif kwa matamshi ya karibuni ya Trump kuhusu mapatano na Iran



Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika katika ukurasa wake wa twitter akijibu matamshi ya karibuni ya Trump kuhusu mapatano na Iran kuwa: " Bwana Trump sisi tumefikia mapatano ya kibinadamu licha ya jitihada hasi zilizofanywa na maafisa wenu. Wakati huo huo tayari tulikuwa tumefikia mapatano hata kabla hujaingia madarakani."

Zarif amesisitiza kuwa: "Iran na washirika wengine ndani ya mapatano ya JCPOA hawajawahi kutoka kwenye meza ya mazungumzo. Washauri wako ambao aghalabu yao umewafukuza wamecheza kamari ya kipumbavu. Hii kwamba ni lini mtachukua uamuzi wa kurekebisha suala hili linakuhusuni nyinyi wenyewe. 

Katika ujumbe wake wa Twitter Donald Trump mbali na kuishukuru Iran kwa  kumuachia huru Michael White mfungwa wa Kimarekani, amewaeleza viongozi wa Iran kwamba: "Msisubiri hadi baada ya kufanyika uchaguzi Marekani ndipo mfikie mapatano muhimu."

Rais wa Marekani anadhani kuwa anaweza kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isalimu amri mbele ya hatua na vitendo vyake vya kijuba ambavyo alivitekeleza kwa baadhi ya nchi za eneo tangu aingie madarakani. Bila shaka Wamarekani sasa wanakabiliwa na kashfa kubwa duniani na nara ya  'hatuwezi kupumua" inayopigwa leo hii na wananchi wa Marekani wakilaani mauaji ya kikatili na ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Mmarekani mweusi wa nchi hiyo yaliyofanywa na polisi mzungu, inadhihirisha uhakika huu wa mambo. 

Hii leo Trump ambaye anakabiliwa na matatizo makubwa ya ndani, maandamano makubwa ya wananchi pamoja na masaibu yanayosababishwa na mlipuko mkubwa wa maambukizi ya virusi vya corona kutokana na uongozi wake dhaifu anazidi kubainikiwa kwamba zama zile za siasa za uonevu na ukandamizaji zimegonga mwamba; na kwamba Marekani haitaweza kujipapatua katika mkwamo huo iwapo haitaachana na siasa zake hizo ghalati.


Ni dhahir shahir kuwa lengo la diplomasia ya Marekani si kufanya mazungumzo bali ni kuyachokoza mataifa mengine. Mapendekezo ya eti kufanya mazungumzo na kufikia mapatano na Iran yaliyotolewa kwa njia ya Twitter ni wazi kuwa yametolewa na akili iliyochanganyikiwa ya rais wa Marekani na washauri wake. Aidha katika Tweet ya Trump ya siku kadhaa zilizopita pia kuna mstari wa wazi uliokolezwa wino wa mwenendo kama huo ambao lengo lake ni kuzipotosha fikra za waliowengi kwamba Marekani inaweza kuiburuza Iran kwenye meza ya mazungumzo. 

Ali Shamkhani Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran pia juzi Ijumaa aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: 'Hali ya Rais Donald Trump wa Marekani iwe ni katika kuamiliana na masuala ya kimataifa, kusimamia vibaya kuenea maambukizi ya corona au hata kushughulikia machafuko makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi yanayoendelea sasa ndani ya Marekani imevurugika kiasi kwamba timu yake haina njia nyingine ghairi ya kubuni na kumdhihirishia mafanikio ya uwongo.'


Hotuba za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi katika minasaba tofauti zinajibu kwa uwazi zaidi kuhusu ni kwa nini mazungumzo hayawezi kufanyika kati ya Iran na Marekani.

 Akizungumzia suala hilo mwanzoni mwa kikao cha darsa ya masomo ya juu kabisa ya fiqhi katika kuanza mwaka wa masomo wa hauza za kielimu tarehe 26 mwezi Shahrivar mwaka 1398, Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alilitaja lengo la viongozi wa Marekani katika mazungumzo kuwa si kufikia utatuzi wa kiuadilifu bali ni kuutwisha upande wa pili matakwa yake ya kijuba na kusema: Siasa za serikali ya Marekani za mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Iran zinatekelezwa katika kalibu ya vikwazo mbalimbali, vitisho na tuhuma zisizo na msingi wowote. Hii ni kwa sababu serikali ya sasa ya Marekani inatambua kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kupigishwa magoti kwa kufanyiwa mujamala au kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa. Aliongeza kuwa ndio maana viongozi wa nchi hii wakawatangazia kwa sauti moja Rais, Waziri wa Mambo ya Nje na wengineo kuwa hawatafanya mazungumzo yoyote na Marekani, si mazungumzo ya pande mbili au ya pande kadhaa." 
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items