Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameeleza wasi wasi iwapo Uingereza kweli ina dhamira ya kufikia makubaliano na Umoja wa Ulaya juu ya kujiondoa kwenye jumuiya hiyo kwa njia sahihi. Kansela Merkel amesisitiza kwamba litakuwa jambo la manufaa kwa kila upande ikiwa Uingereza itajiondoa katika msingi wa mkataba.
Kiongozi huyo wa Ujerumani ameeleza kuwa lengo hilo linaweza kufikiwa iwapo tu, pande zote zitashirikiana kwa dhati. Amesema jambo la msingi ni kutambua hali halisi na siyo matamanio ya kila upande kwa usemi mwingine siyo kile ambacho Uingereza inakitaka.
Bibi Merkel ameeleza wazi kwamba ikiwa serikali ya Uingereza inataka kuufafanua uhusiano wake na Umoja wa Ulaya, namna inavyotaka, basi itapaswa kuishi na matokeo ya uhusiano huo kwa maana kwamba hapatakuwapo uhusiano wa karibu, kiuchumi.
Uingereza ilijiondoa rasmi Umoja wa Ulaya tarehe 31 mwezi Januari lakini imebakiwa na muda wa miezi sita kufikia mkataba na Umoja wa Ulaya. Baada ya hapo sheria za Umoja huo hazitatumika tena nchini Uingereza.
