Jun 30, 2020

Mwanamuziki maarufu wa Ethiopia auawa kwa kupigwa risasi

  Muungwana Blog 5       Jun 30, 2020
Maandamano makubwa yamezuka nchini Ethiopia kufuatia mauaji ya mwanamuziki Hachalu Hundessa, aliyepata umaarufu kutokana na nyimbo zake za kisiasa.

Watu wawili wamefariki wakati wa maandamano hayo katika mji mmoja, madaktari wameiambia BBC.

Nyimbo za Hachalu zilikuwa zinaangazia haki ya jamii ya Oromo na zilitumiwa sana katika msururu wa maandamano yaliyochangia kuondoka madarakani kwa waziri mkuu aliyekuwepo wakati huo.

Muimbaji huyo aliyekuwa na umbri wa miaka 34 alikuwa amesema kwamba amepokea ujumbe wa kumtishia maisha.

Maelfu ya mashabiki wake walielekea katika hospitali ya Addis Ababa ambako mwili wa muimbaji huyo ulipelekwa usiku wa Jumatatu, anasema mwandishi wa BBC Afaan Oromo, Bekele Atoma.

Kwao, alikuwa sauti ya kizazi ambacho kinapinga unyanyasaji wa miongo kadhaa wa serikali dhidi yao, alisema.

Polisi walitumia vitaza machozi kutawanya makundi ya watu.

Milio ya risasi ilisikika mjini Addis Ababa huku wakichoma moto magurudumu ya magari.

Katika eneo la mashariki mwa mji wa Chiro, watu wawili walipigwa risasi na kuuawa wakati wa maandamano, mhudumu wa afya katika hospitali moja mjini humo ameiambia BBC Idhaa ya Oromo.

Katika mji mwingine - Adama - mtu mmoja alijeruhiwa na jengo la serikali kuteketezwa.

Huduma za intaneti zimefungwa katika baadhi ya maeneo nchini humo huku maandamano yakisambaa hadi maeneo mengine ya jimbo la Oromia.

Mwili wa Hachalu umepelekwa katika mji wa Ambo, karibu kilomita 100 (maili 62) magharibi mwa mji mkuu wa Addis Ababa.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed ametuma rambi rambi zake katika mtandao wake wa Twitter akisema kuwa Ethiopia "imepoteza kiungo muhimu siku ya leo" na kutaja tungo zake kuwa "nzuri sana".

Oromo ni kabila kubwa zaidi nchini Ethiopia, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likilalamikia kutengwa kisiasa na kiuchumi.

Maandamano ya kutaka mageuzi yalizuka mwaka 2016 dhidi ya serikali.

Muungano wa chama tawala hatimaye ulifanya mageuzi na kumuondoa madarakani - Waziri Mkuu wakati huo Hailemariam Desalegn na kumteua Dkt Abiy ambaye anatokea kabila la Oromo.

Amefanya msururu wa mageuzi ambayo yamebadilisha taifa hilo ambalo lilitajwa kuwa la kikatili.

Alishinda tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019 katokana na juhudi zake za kuleta amani sio tu baina ya Ethiopia na hasimu wake wa jadi Eritrea lakini pia juhudi zake za kuleta mageuzi Ethiopia zilitambuliwa.
logoblog

Thanks for reading Mwanamuziki maarufu wa Ethiopia auawa kwa kupigwa risasi

Previous
« Prev Post