Mwandishi habari aliyechochea maandamano ya 2017 ya Iran ahukumiwa kifo


Mahakama nchini Iran imemuhukumu kifo mwandishi mmoja wa habari ambaye kazi ya mtandaoni ilisaidia kuhamasisha maandamano ya nchi nzima dhidi ya hali ngumu ya kiuchumi mwaka 2017.

Mwandishi huyo, Ruhollah Zam, alikuwa amerejea Iran katika mazingira yasiyofahamika na kisha akawekwa kizuizini. Msemaji wa mahakama, Gholamhossein Esmaili, ametangaza hukumu hiyo leo.

Mwandishi huyo wa habari alikuwa akiendesha tovuti iitwayo AmadNews, ambayo ilituma picha za vidio na taarifa zilizokuwa zikiwakosoa vikali maafisa wa Iran. Wakati huo alikuwa akiishi na kufanya kazi zake mjini Paris, Ufaransa, kabla ya kushawishiwa kurejea Iran, ambako alikamatwa mwezi Oktoba mwaka jana. Zam alijitokeza baadaye kwenye televisheni ya umma, akikiri na kuomba radhi kwa makosa aliyofanya.

 Zam ni mtoto wa ulamaa wa Kishia, Mohammad Ali Zam, mwanamageuzi aliyehudumu kwenye serikali mwanzoni mwa miaka ya 1980, lakini mwezi Julai 2017 aliandika barua ya kukana harakati za mwanawe mitandaoni.