UN: Janga la corona linarudisha nyuma juhudi za kukomesha ndoa za watoto na ukeketaji


Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, janga la corona linarudisha nyuma maendeleo yaliyopatikana katika jitihada za kukomesha ndoa za watoto na ukeketaji wa uke (FGM), suala ambalo linahatarisha hatma ya mamilioni ya wasichana katika pembe mbalimbali duniani.

Mkuu wa Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) Natalia Kanem amesema kuwa, ugonjwa wa COVID-19 unaifanya kazi ya shirika hilo kuwa ngumu kwa sababu wasichana wengi sasa wako hatarini.

UNFPA imesema kuwa, wasichana wengine milioni 13 wanaweza kuolewa mapema na milioni mbili zaidi wanaweza kukeketwa katika muongo mmoja ujao jambo ambalo ni kinyume na matarajio ya hapo awali. Limesisitiza kuwa ugonjwa wa COVID-19 unavuruga juhudi za ulimwengu za kukomesha vitendo hivyo.

Taarifa ya UNFPA pia imeongeza kuwa, umaskini mkubwa unaosababishwa na janga hilo unaweza pia kushinikiza wazazi zaidi kuwaoza mabinti zao mapema.

Ripoti hiyo imesema wasichana wapatao 33,000 wanalazimishwa kufunga ndoa mapema kila siku aghlabu kwa wanaume wazee, na inakadiriwa kuwa milioni 4.1 wako katika hatari ya kukeketwa mwaka huu wa 2020.